MUTUA: Tupuuze habari potovu kuhusu chanjo za corona

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI leo hii ukiambiwa chanjo ya corona imefika nchini Kenya na Serikali itaitoa bila malipo, utatunga foleni kuipata au utakimbia kama mtu aliyeona joka?

Nakuuliza kwa kuwa nimesikia mengi yakisemwa dhidi ya chanjo za ugonjwa huo ambazo tayari zinatolewa kwingineko duniani, masikioni mwangu yakasikika kama hekaya tu.

Kumbuka hekaya zote za kale zilizokusawiria mazimwi yakiwameza watoto zilikuwa za uongo; zilinuiwa kukuonya dhidi ya tabia fulani.

Hivyo ndivyo makuzi ya watoto yalivyo, jamii haiishi kutafuta mbinu za kuzuia utundu. Dhamira kuu huwa ni kuwafunza kuhusu manufaa ya nidhamu na adhabu ya upotovu.

Lakini hata hizo hadithi za mazimwi na mbinu nyingine za kuwafunzia watoto zina mwisho wake. Huwezi kumhadaa binadamu siku zote.

Sisi si watoto tena, hivyo ni lazima tuambiwe ukweli kuhusu kila kitu tunachohusishwa nacho ili tukabiliane na uhalisia wa mambo, uwe wa heri au shari.

Nimemsikia Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, akiwaonya watu wake dhidi ya chanjo ya corona, sikwambii hata amedai ni njama ya wazungu kuwamaliza Waafrika.

Si Magufuli pekee, nimewasikia watu wengi tu, hasa Waafrika, wakisema mambo ya kuaibisha kuhusu chanjo mbalimbali za ugonjwa huo ambazo tayari zimeanza kutolewa.

Naam, mambo ya kutia aibu kwani kuna mambo unayoweza kusema mbele ya watu, wakaulizana ulikwenda shule kufanya nini ikiwa fikra zako zingali kiwango hiki!

Baadhi hupuuzilia mbali na hata kulaani uvumbuzi wa kisayansi uliofanyiwa majaribio tosha ilhali hawachelewi kukimbilia ugangani kupigiwa bao; sarakasi za kubabaisha tu!

Magufuli na wengine wanaotuonya dhidi ya chanjo za corona wanasema huenda ni njama ya ama kumwangamiza Mwafrika mara moja au kumnyima uwezo wa kuzaliana.

Na wanaweza kukushawishi haraka ukiwasikiza sana kisha ukose kufanya utafiti wa kina ili kujua ukweli.

Mathalan, wanauliza iwapo wanasayansi wa mataifa yanayoendelea ni wakali sana, kwa nini bado hawajapata chanjo za ukimwi, malaria na maradhi mengine ya kuambukiza?

Ukisikia hayo unatikisa kichwa kidogo kukubaliana nao, na hapo ndipo unapompa fursa mganga asiyejua kitu kukuhadaa na kukupa suluhisho asilonalo kabisa!

Ukweli ni kwamba maradhi mengine hayo, sawa na corona tu, yamekuwa yakibadilikabadilika, hivyo tafiti za chanjo zake ni kazi ya kuendelea.

Baadhi ya wanaoeneza uvumi dhidi ya chanjo za corona hata wanadai zinatengenezwa kwa vijusi na uchafu mwingine usioandikika hapa.

Ukiwa na akili unajiuliza zimetunguliwa mimba ngapi duniani ili kupata mamilioni ya chanjo ambazo tayari zinatolewa. Uongo mtupu!

Lakini uongo huo si wa kwanza; tangu zamani watu wametafuta sababu za kukiharibia sifa kitu wasichokipenda wala kukielewa.

Iwapo chanjo ya korona itafika Afrika, mwenzangu ikimbilie kama chakula cha msaada kinavyokimbiliwa na hata kupiganiwa wakati wa kiangazi. Tia bidii uishi.

mutua_muema@yahoo.com

Habari zinazohusiana na hii