MWANAMUME KAMILI: Karibu kijiweni tuwakemee wanaotafuta “kulikopikwa”

Na DKT CHARLES OBENE

KAULI kwamba wanaume wa leo “wanabahatisha tu maisha” imevuma kwenye midomo ya vimwana kwa muda.

Sijui kama kweli wanaume “wanabahatisha tu maisha.” Nijuavyo ni kwamba kuna wanawake kwa wanaume wanaoishi mfano wa nyani wanaoruka kutoka mti mmoja hadi mwingine kutafuta tu kivuli na matunda mabivu! Karibu kijiweni tuwakemee hawa mahambe wanaotafuta “kulikopikwa” wala hawana haja “kwenda shambani kuatika mbegu, kupalilia miche na kusubiri mabichi yakawa matunda mabivu!” Kwani sivyo wanavyoishi mwanamke kwa mwanamume kamili?

Hilo la wanaume kubahatisha maisha ndio kwanza mwiba kwenye ndoa nyingi za “mastaa na viongozi tajika” zinazotika mfano wa debe tupu. Nazungumzia hizi kero za “mastaa na viongozi tajika” wanaooa na kuolewa kwa harusi zilizojaa mbwembwe kisha kufika mitandaoni wiki moja baadaye kutangaza talaka! Tuliweke wazi kwamba hizi “ndoa za kamera na picha kwa umma” zinadunisha mno hadhi ya wangwana wanaojua maana ya “mke na mume kuwa kitu kimoja!

Madume na majike wanaooa na kuolewa kwa wiki ama mwezi mmoja wanalaumu “tabia kinzani,” “ufasiki wa wanaume”, “ufukara wa madume” kama vijisababu vinavyochochea hizi talaka za mitandaoni. Sio siri kwamba tunao “wanaume fukara” wasioweza timizia mke mahitaji. Wako vilevile madume wasioacha kuku akala mtama na kwenda zake. Lakini nani asiye kasoro japo moja? Lawama za majike wa leo ni vijisababu tu. Dhamira ya mtu haina kamba mwanadamu kumvuta kwa lazima. Tunaweza badili misitu lakini nyani ni nyani tu!

Mitandao ya umma imejaa nyaraka za majike wanaotetema na kukereka juu ya “ufasiki wa wanaume wa leo. Kinaya ni kwamba hawa wanaoteta juu ya “ufasiki wa wanaume” wameolewa kama mke nambari tatu ama nne! Isitoshe, ni watoto waliolelewa kwenya makazi ya “kuni mekoni” sisemi “maji ya mto!” Ndio dunia ya leo hiyo! Kila mwamba ngoma anavutia kwake.

Waasisi wa tetesi hizi wanashikilia kwamba wanaume wa leo wanafuata upepo tu pasipo ari wala mshawasha kutafuta mali na hali inayofurahisha mke na wanao. Sio siri tena kwamba baadhi ya wanawake wanaona heri kukumbatia “upweke” badala ya “kufungwa minyororo kwenye ndoa na malofa wasiomfaa mke kitu.” Warembo wamesonga hatua mbele zaidi. Wameona heri “kutafuta na kulea watoto wao wenyewe” pasipo kutegemea hali na mali ya mwanamume wa leo. Hawajachoka kina dada hawa. Wamesonga hatua maradufu. Wameona afadhali mke kununua kipande chake cha ardhi akajenga nyumba yake mwenyewe! Mwenda omo na tezi marejeo ngamani!

Hongera nyie mnoajizatiti kufungua “minyororo ya ndoa” na kutafuta maisha yenye uhuru huria bila bughudha na kero za hawa mahambe wanaoitwa “wanaume!” Kila mtu ana haki kutoa hoja, kufuata ndoto na kuishi kwa msingi wa maadili anayoamini mwenyewe! Maadamu mtu anazo akili, anaridhiwa kuchagua maisha anayotaka mwenyewe. Linalokera moyoni ni tabia ya walevi kupatana kwenye mabaa, kuolewa pasipo mikakati ya kudumisha ndoa kisha kufika mitandaoni na hizo “nyaraka za talaka!”

Mwanamtu ulitarajia nini ulipoacha gumegume likutambalie, likutandazie misuli kabla hata wewe kujua usuli wake? Kuna hawa vimwana wa leo wanaochemka mili mfano wa samli tena wasioona aibu kufuata walevi na kuwaita “wanaume!” Nguzo za mke ni mbili: hadhi na hekima! Ukivuliwa hadhi huna budi kutumia hekima. Ukikosa yote basi shikilia mpini kimyakimya na kulilima hilo shamba la mawe ulilotaka mwenyewe. Maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga.

Msomaji mpendwa hebu tathmini kwa kina utueleze jinsi hali ilivyo kwako! Wewe ni mwanamke ama mwanamume wa aina gani? Lipi unalofanya kufanikisha ndoa na kukuza familia yako? Unatoa mchango gani ili kuzikabili changamoto zinazotishia umoja wa familia? Unachumia wapi angalau kopo kwa wanao? Unachangia nini kwenye hazina ya familia? Ewe mja na akili zako razini, unafanya nini kusitisha tabia za nyani wanaoruka kutoka mti mmoja hadi mwingine kutafuta tu kivuli na matunda mabivu?

Licha ya hizi sarakasi za “mastaa tajika na viongozi” wanaooa na kuolewa kila mara, bado kuna familia za wangwana zilizotulia na ambazo zinaendesha mambo yao kwa misingi ya umoja na muamana unaohimizwa kwenye vitabu vitakatifu. Ole nyinyi mnaotafuta “watoto na mali” katika “makazi” yenu wenyewe. Wenzenu wanaishi kwa furaha kama mwili na nafsi moja. Ujana ni moshi! Mwenda omo na tezi marejeo ngamani. Mtafukuza upepo na mwishowe tutapatana “ngamani!” Mtu ni utu na utu ni kuishi kama mwanamke na mwanamume kamili.

obene.amuku@gmail.com 

Habari zinazohusiana na hii