• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
UMBEA: Unaweza chagua kutopendwa ila kumbuka huishi kisiwani!

UMBEA: Unaweza chagua kutopendwa ila kumbuka huishi kisiwani!

Na SIZARINA HAMISI

UMESHAWAHI kujikuta katika maisha ambayo umezungukwa na watu wasiokupenda? Kiasi kwamba wanajionyesha wazi katika maneno, matendo na mienendo yao?

Pamoja na kwamba wakati mwingine inaweza kuwa wanafanya hivyo bila sababu yoyote ya msingi, wakati mwingine pia mwenendo na tabia yako huenda ndivyo vinavyochangia usipendwe na watu. Hivyo kama unataka ufahamu sababu inayofanya watu wasikupende, tathmini haya yafuatayo:

Jinsi unavyopenda kusikilizwa, ndivyo watu wengine wanavyopenda kusikilizwa. Ikiwa huna muda wa kusikiliza mawazo, changamoto ama mtizamo wa watu wengine, nao pia hawatakuwa na muda wa kukusikiliza na hata wakikusikiliza huenda ikawa wamelazimika kufanya hivyo. Hivyo siku zote thamini mtizamo na mawazo ya watu wengine kama vile unavyothaminiwa.

Iwapo umetawaliwa na “umimi” kupitiliza na kuwa ni mtu mwenye majivuno, ni mara chache utapata watu wakikupenda ama kukuelewa. Ni muhimu wakati mwingine kujali na kuthamini yale ya watu wengine. Halafu wapo wale wenye upendeleo wa wazi. Mara nyingi ukiwa mtu mwenye upendeleo utachukiwa na watu wengi ambao hawajapata nafasi ya kupendelewa nawe. Tabia hii ya upendeleo pia huleta mgawanyiko, iwe katika familia, jamii ama maeneo unayojumuika na watu wengine. Haki ni msingi wa kuishi vizuri na kila mtu.

Kwa upande mwingine, ni vyema kuzungumza na kila mtu. Iwe mtu huyo anao uwezo wa kukusaidia ama la. Iwapo unayo tabia ya kuchagua watu wa kuzungumza nao, unazungumza na mtu pale unapokuwa na shida na wakati mwingine ukikutana naye unapishana naye kama gogo, basi utachukiwa. Iwapo unahitaji ueleweke ama upendwe na watu wengine, zungumza nao hata kama huna shida nao.

Tabia ya kusengenya na kusema vibaya watu wengine ni sawa na kupandikiza sumu. Kwani mara nyingi yale unayosema kuhusu mtu ama watu wengine huwarudia tena wahusika na mara nyingi yule msambazaji wa hizo kauli pia hujulikana. Iwapo una hasira ama uchungu na mtu mwingine, mweleze usoni mwake na sio kwa watu wengine.

Wapo waliosema mkono mtupu haulambwi. Na hivi ndivyo ilivyo kwa watu. Usiwe una mazoea ya kuweka maneno maneno kila wakati, inapobidi weka vitendo. Usiwe mchoyo wa mazuri yako, wanufaishe pia na wengine pale unapoweza. Siku zote mchoyo hana rafiki.

Hekima ya kutawala kinywa chako ni muhimu sana. Inawezekana unazungumza ovyo ama yasiyofaa kwa watu, unapayuka bila utaratibu na bila kujali unayosema yanaweza kumdhuru ama kumuumiza mtu mwingine. Iwapo hii ni tabia yako, sio rahisi kuwa na uhusiano mzuri na wengi na bila shaka wengi pia watakuchukia. Siku zote jitahidi kutawala kinywa chako na yale yote yanayotoka kwa maneno.

Pamoja na kwamba unaweza kuchagua kuishi kwa kutopendwa na mtu ama watu, ukumbuke pia kwamba huishi katika kisiwa na unaoishi nao ni binadamu.

[email protected]

You can share this post!

FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza ubongo wa mtu...

Corona yatulia kupisha siasa