• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Ibrahimovic na Lukaku wapigwa marufuku ya mechi moja kila mmoja kwa utovu wa nidhamu

Ibrahimovic na Lukaku wapigwa marufuku ya mechi moja kila mmoja kwa utovu wa nidhamu

Na MASHIRIKA

MAFOWADI Zlatan Ibrahimovic na Romelu Lukaku wamepigwa marufuku ya mechi moja kila mmoja baada ya kudhihirisha utovu wa nidhamu wakati wa gozi la Coppa Italia lililowakutanisha AC Milan na Inter Milan mnamo Januari 26, 2021.

Ibrahimovic wa AC Milan alipigwa marufuku baada ya kufurushwa ugani kwa kuonyeshwa kadi mbili za manjano, mojawapo ya kadi hizo ikichangiwa na makabiliano makali kati yake na Lukaku wa Inter uwanjani.

Lukaku pia alionyeshwa kadi ya manjano katika mechi hiyo na atapigwa marufuku kwa sababu hiyo ilikuwa mara yake ya pili kulishwa kadi hiyo kwenye kampeni za Coppa Italia muhula huu.

Ingawa hivyo, Ibrahimovic amekana kumrushia Lukaku cheche za matusi wakati wa mechi hiyo, jambo ambalo kwa sasa litachunguzwa na vinara wa Shirikisho la Soka la Italia.

“Katika historia ya maisha ya Zlatan, hapajawahi kutokea kisa cha ubaguzi wa rangi. Isitoshe, hakuna nafasi kwa matusi,” akaandika Ibrahimovic kwenye akaunti za mitandao yake ya kijamii.

Ibrahimovic na Lukaku wote walifunga bao kwa upande wa waajiri wao katika gozi hilo lililochezewa uwanjani San Siro kabla ya kiungo Christian Eriksen wa Inter kutokea benchi na kuvunia kikosi chake ushindi kupitia frikiki ya mwisho wa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Antonio Conte, Inter waliibuka na ushindi wa 2-1 katika mechi hiyo.

You can share this post!

Corona yatulia kupisha siasa

Gor Mahia wasajili fowadi matata Fonseca kutoka Brazil