TAHARIRI: Tuwazie kukuza mbio fupifupi pia

KITENGO CHA UHARIRI

MAREHEMU Nicholas Bett aliponyakulia Kenya medali nadra ya dhahabu kwenye Riadha za Dunia za Beijing mnamo 2015, Wakenya hawakufurahia ushindi huo tu kwa sababu ya kuipata medali katika fani ambayo taifa hili halifanyi vyema, bali pia kwa sababu nishani hiyo adimu ingewezesha nchi hii kumaliza mashindano hayo katika nafasi bora zaidi.

Waama, mwaka huo Kenya iliibuka mshindi wa jumla duniani kwenye mashindano hayo ambayo yametawaliwa na Amerika, Urusi na Uchina kwa muda mrefu.

Marehemu Bett alichangia pakubwa kwa taifa hili ‘dogo’ kushinda ulimwengu mzima katika mashindano hayo ya kimataifa baada ya kutawala mbio za mita 400 za kuruka viunzi.

Wala hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mkimbiaji wa Kenya kung’aa katika mbio fupifupi kwenye medani ya kimataifa. Wapo wakimbiaji wa Kenya akiwemo babaye jagina David Rudisha, Daniel, waliowahi kung’ara katika mbio za masafa mafupi hapo awali.

Je, tujifunze nini kutokana na ufanisi huu wa Bett? Sharti tuanze kuangazia ukuzaji wa vipawa vya wakimbiaji wa mbio fupifupi.

Tujiulize, je ni kwa sababu gani hatuna wakimbiaji wa mita 100, mita 200, mita 100 kuruka viunzi na hata mara nyingi kukosa wale wa mita 400, na mita 400X4 za kupokezana vijiti?

Twafaa kujisaili iwapo tunafanya vyema kwa kuzamia tu mbio za masafa ya wastani na marefu. Je, itakuwaje iwapo tutaimarisha mbio za masafa mafupi? Mataifa mengi shindani hutupita kwa jumla ya medali kutokana na kushiriki fani nyingi za riadha hizi.

Kama tuliweza kuibuka kidedea mwaka wa 2015 kwa kushiriki tu mbio za masafa ya wastani na marefu, kisha ‘tukaokota’ nishani mbili za kubahatisha katika urushaji mkuki na mita 400 za viunzi, sembuse tukichukulia kwa uzingativu zaidi mbio fupifupi?

Tumechochewa kuyaandika maoni haya na tukio la hivi majuzi ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Ferdinand Omanyala aliandikisha muda wa kasi zaidi nchini humu katika mbio za mita 100 alipokurupuka kwa sekunde 10 pekee.

Hiyo ni ishara tosha kuwa iwapo talanta hizi zitatambuliwa mapema na kuanza kustawishwa, Kenya itaanza kushindana na Amerika, Jamaica na mataifa mengine ya mabara ya Amerika ambayo yamekuwa yakitawala mbio hizo.

Kwa kufanikisha hilo, ipo hakika kuwa taifa hili litaanza kutawala mashindano yoyote ya kimataifa yenye fani ya mbio.

Habari zinazohusiana na hii