• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Aibu wabunge wakilimana makonde mazishini

Aibu wabunge wakilimana makonde mazishini

Na SAMMY WAWERU

Hafla ya mazishi ya babake Naibu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi, Mzee Abel Gongera Jumatatu iligeuka kuwa ukumbi wa mangumi na makonde baada ya wabunge wawili kukabana.

Kwenye picha na video zinazosambaa mitandaoni na kuangaziwa na pia vyombo vya habari, mbunge wa Dagoretti Bw Simba Arati na Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini), wameonekana wakishikana mashati.

Arati akizungumzia waombolezaji amenukuliwa akimkashifu Naibu wa Rais, William Ruto ambaye pia alikuwa katika hafla hiyo ya mazishi.

Mbunge huyo anaskika akisema “kuna jamii mbili nchini ambazo zimetawala kwa muda mrefu na umewadia wakati zizipe jamii zingine nafasi pia ziwe uongozini”.

Aidha, Bw Arati anaskika akimtaja Dkt Ruto na Bw Osoro ambaye ni mwandani wa Naibu Rais.

Kwenye video, waombolezaji wanaskika wakimzomea Arati, na ghafla jukwaa linageuka kuwa ukumbi wa vita, kati ya Arati na Osoro, maafisa wa polisi wakilazimika kuingilia kati.

Hii ni ishara ya jinsi joto la kisiasa nchini linaendelea kupanda, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Ruto wakionekana kutofautiana hadharani.

Majuma kadha yaliyopita, Rais Kenyatta aliashiria kutomuunga mkono Dkt Ruto kumrithi 2022, kinyume na ahadi zao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto aliweka wazi kwamba hatarajii kuungwa mkono na Rais kuingia Ikulu, akionekana kuwajibu wanaodai Rais Kenyatta ana deni lake la kisiasa.

Matamshi ya Arati kuhusu jamii ambazo hazijawahi kuwa mamlakani kupewa fursa, yanawiana na ya Rais Kenyatta aliyotoa mapema Januari 2021.

You can share this post!

TANZIA: Simeon Nyachae afariki

Sonko aandamana na wakili wake hadi afisi za DCI