• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Siasa za Raila, UhuRuto zatishia amani

Siasa za Raila, UhuRuto zatishia amani

NA BENSON MATHEKA

MIENENDO ya wanasiasa wakuu nchini kuhusu mpango wa BBI na uchaguzi mkuu wa 2022, inatishia kutumbukiza Kenya kwenye ghasia sawa na za 2007.

Hii ni kutokana na matukio ya hivi punde katika mikutano ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ambayo yanatoa dalili kwamba tofauti za viongozi hao wawili zinaweza kuchoma nchi hii kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hapo jana ghasia zilizuka kwenye mazishi ya babake Naibu Gavana wa Kisii, Joash Maangi wakati wanasiasa na wafuasi wa Dkt Ruto na Bw Odinga walipopigana na kutatiza shughuli hiyo ya maombolezo.

Hii ilitokea siku chache tu baada ya ghasia za wiki jana katika soko la Githurai, Kaunti ya Kiambu wakati wa mkutano wa Bw Odinga na siku iliyofuatia katika soko la Burma jijini Nairobi kwenye mkutano wa Dkt Ruto.

Mnamo Jumapili akiwa Sagana katika Kaunti ya Nyeri, Rais Uhuru Kenyatta alikosa kulaani ghasia hizo, na badala yake akasema wanaotaka kuzua fujo watakabiliwa kwa fujo pia.

“Tumekaa miaka hii yote na amani. Sasa unaona mtu anasema hii ni ‘territory’ yangu, halafu mnatupia Raila mawe Githurai. Unafikiria hata yeye hana vijana? Si mliona ile ilitokea the next day! Kama ni mawe, tupa nitupe! Asijaribu kutumia kifua hapa. Hakuna mtu hana huo uwezo,” akasema rais akimrejelea naibu wake.

Ni kutokana na matukio haya ambapo viongozi wa kidini na wachanganuzi wa siasa wanaonya kuwa wanasiasa wakuu wanapalilia mazingira ya ghasia.

Hatari ya 2007 kujirudia

“Kuna hatari ya Kenya kujipata ilipokuwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 uliotanguliwa na kura ya maamuzi iliyogawanya Wakenya kama inavyofanyika sasa. Wanavyofanya wanasiasa kwa wakati huu ni kupiga ngoma za vita mapema miezi 17 kabla ya uchaguzi mkuu,” asema mdadisi wa siasa Keith Muumbo.

Bw Muumbo anasema ikiwa hali iliyoshuhudiwa jana katika mazishi ya Kisii na wiki jana Nairobi na Kiambu itaendelea, Kenya itavurugika.

Ghasia ambazo zinashuhudiwa kwa sasa zinachochewa na matamshi ya kisiasa ya viongozi hao na washirika wao.

Bw Odinga amekuwa akitaja kampeni ya ‘hasla’ ya Dkt Ruto kama ‘takataka’ na kumuita ‘mwizi wa mali ya umma’, naye Dkt Ruto amekuwa akimuita ‘mlaghai’ na ‘mganga’.

Wadadisi wanasema tofauti na 2007 ambapo ghasia zilichochewa na chuki za kikabila, wakati huu kuna chuki za matabaka kati ya maskini na wanaochukuliwa kuwa wenye mali.

“Taharuki inayotokota kwa sasa sio ya kati ya jamii tofauti. Ni kati ya matabaka. Kuna mbegu ya chuki za tabaka inayopandwa miongoni mwa maskini kwamba wamekosa kufanikiwa kwa sababu haki zao zimekaliwa na matajiri na familia zenye ushawishi. Mbegu hii inaweza kukomaa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 au kabla na kutumbukiza nchi kwenye ghasia,” asema Bw Muumbo.

Majuma mawili yaliyopita, waendeshaji wa bodaboda katika Kaunti ya Nakuru walichoma gari la mfanyabiashara mmoja wakimlaumu kwa kutoka familia ya walio nacho. Visa kama hivi vimeripotiwa maeneo tofauti.

You can share this post!

Uhuru sasa awategemea Raila, Kalonzo na Mudavadi kuvumisha...

Wanaopinga BBI ni wanafiki – Raila