• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Kansa ya lango la uzazi bado changamoto mashambani

Kansa ya lango la uzazi bado changamoto mashambani

NA PAULINE ONGAJI

Alipogunduliwa kuwa anaugua kansa ya lango la uzazi, mwanzoni Milka Kavere, 61, mkazi wa kijiji cha Muhudu, Kaunti ya Vihiga, hakujua cha kufanya kwani hakuwa na ufahamu mwingi kuhusu maradhi haya.

Hii ilikuwa Februari 2020 ambapo baada ya kuenda hospitalini ili kutibiwa kwa kile alichodhani kuwa ugonjwa wa kawaida, ilibainika kwamba alikuwa katika awamu ya 3C ya maradhi haya.

Hatua yake ya kwenda hospitalini ilitokana na maumivu ambayo alikuwa ameshuhudia kwa muda ila akawa anayapuuza.

“Mara ya kwanza kugundua kwamba mambo hayakuwa sawa, nilishuhudia damu ikitoka ukeni. Hii ilinishangaza sana kwani kitinda mimba wangu ana miaka 20 sasa, na mara ya mwisho kuona hedhi ilikuwa takriban miaka 15 iliyopita,” aeleza.

Kulingana naye, hii ilifuatiwa na uowevu wa rangi ya hudhurungi uliokuwa ukiandamana na harufu mbaya. “Baada ya muda mfupi tena, nilianza kushuhudia uowevu mweupe ambao pia ulikuwa na harufu mbaya,” aeleza.

Ili kudhibiti hali hii alianza kuvalia visodo, lakini bado hakuona dharura ya kumuona daktari. Hata hivyo, haikuwa muda kabla ya ishara hizi kuandamana na maumivu makali ya tumbo na mgongo, vile vile kutapika. Na hapo akalazimika kwenda hospitalini.

“Nilipoenda hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi, nilipatikana naugua kansa ya lango la uzazi, ambapo kulingana na daktari tayari ilikuwa imeenea,” aeleza.

Kilichofuatia kilikuwa ni msururu wa ziara katika hospitali mbalimbali maeneo yaVihiga, Kakamega, Eldoret na hatimaye kituo cha Texas Cancer Center jijini Nairobi, ambapo Julai 2020 safari yake ya matibabu iling’oa nanga.

“Nimefanyiwa mchanganyiko wa matibabu ikiwa ni pamoja na brachytherapy, tibakemia na tibaredio,” aeleza.

Kwa sasa hali yake inazidi kuimarika ikilinganishwa na alivyokuwa mwanzoni. Lakini bado haijabainika ikiwa amepona au matibabu aliyopokea yalitosha kuangamiza kabisa seli za kansa, au la.

“Tatizo ni kwamba Desemba 17 mwaka jana, nilikuwa nimepangiwa kusafiri hadi jijini Nairobi kurejea hospitalini ili kukaguliwa na daktari na kisha kupeleka matokeo katika hospitali ya Hamisi Sub County Hospital na kuendeleza matibabu yangu hapa karibu. Lakini ukosefu wa pesa umenizuia kufanya hivyo,” aeleza.

Anasema maradhi haya yamefyonza pesa na rasilimali chache walizokuwa nazo. “Mume wangu aliuza ng’ombe tisa tuliokuwa nao ili kugharimia matibabu yangu ambapo kufikia sasa tumetumia zaidi ya Sh200, 000, kando na gharama zingine ndogo ndogo,” aongeza.

Mbali na matibabu, gharama yao ya maisha, imeongezeka. “Kwa mfano, daktari alinishauri kuhakikisha kwamba nadumisha lishe bora. Lazima nile nyama nyeupe, mayai na maziwa kila wiki na hii ni ghali mno kwa wakulima wadogo kama sisi,” aeleza.

Ni hali ambayo imewaongezea umaskini kiasi kwamba miradi waliyokuwa nayo imesimama.

“Kuna mwanangu aliyekuwa katika chuo kikuu na ambaye alilazimika kukatiza masomo kutokana na ukosefu wa pesa,” aeleza.

Huku akiendelea kusubiri angaa iwapo atapata senti za kurejea hospitalini, anatumai kwamba matibabu aliyopokea yalitosha kudhibiti maradhi haya na kwamba kansa hii haiendelei kusambaa.

Kulingana na shirika la GLOBOCAN, mwaka wa 2018, kansa ya lango la uzazi iliorodheshwa ya tatu miongoni mwa saratani zilizokithiri sana miongoni mwa wanawake duniani. Inakadiriwa kwamba, kila mwaka visa 569,847 vipya vya maradhi haya vinasajiliwa, huku wanawake 311,365 wakifariki kutokana na ugonjwa huu.

Hapa nchini, inakadiriwa kwamba kila mwaka kuna visa vipya 5,250 vya maradhi haya yanayoorodheshwa ya pili baada ya kansa ya matiti, saratani zilizokithiri miongoni mwa wanawake kati yaumri wa miaka 15 na 44.

Japo takwimu kamili kuhusu maradhi haya katika maeneo ya mashambani bado sio dhahiri, wataalamu wanahoji kwamba huenda kansa ya lango la uzazi ikawa tishio kwa wanawake wengi wanaoishi mbali na miji mikuu, huku tatizo la utambuzi wa mapema likijitokeza

Eunice Javoga, mtafiti msaidizi na mratibu katika shirika lisilo la kiserikali la Ampath Oncology katika hospitali ya Hamisi Sub-County Hospital anasema utamaduni ni mojawapo ya vizingiti vikuu katika vita dhidi ya maradhi haya.

“Wanawake wanaoishi katika maeneo ya mashambani bado wameshikilia sana utamaduni unaowapa waume zao mamlaka dhidi ya afya yao. Kwa mfano, ili kufanyiwa uchunguzi wa kansa ya lango la uzazi ambao mara nyingi huhusisha sehemu za uzazi kukaguliwa, lazima mumeo akupe ridhaa, na mara nyingi huwa wanakataa.”

Na hata kwa wale wanaokubali kufanyiwa, anasema pindi wanapogundulika kuugua maradhi haya, wanatoweka kutokana na unyanyapaa unaohusishwa na ugonjwa huu, na hivyo kusababisha kuchelewa katika utambuzi wa mapema wa kansa ya lango la uzazi.

Lakini tatizo la ukosefu wa pesa ndilo limeonekana kuwa tishio kubwa hata zaidi. “Ukosefu wa fedha unachangia pakubwa kwani wanawake wengi katika maeneo ya mashambani wanatoka katika familia maskini, na hata kuja hospitalini ni gharama ambayo wengi hawawezi kumudu. Kwa wale wanaofanikiwa kufika hospitalini na kufanyiwa uchunguzi, changamoto ya kufuatilia matokeo ni kubwa pia kutokana na sababu za kiuchumi,” aeleza.

Hii imekuwa changamoto katika vita dhidi ya maradhi haya ambayo ufanisi wa matibabu yake unategemea na iwapo yatatambuliwa mapema au la.

Kulingana na Dkt Gregory Ganda, mwanajinakolojia wa onkolojia katika Kaunti ya Kisumu, wagonjwa wengi wa kansa ya lango la uzazi katika maeneo ya mashambani hugundulika katika awamu ya 3, wakati ambapo seli za kansa zimeenea kwenye lango la uzazi na hata kuanza kuingia katika tishu za sehemu hii.

“Kumbuka kuwa hii ni mojawapo ya kansa hatari mno ambapo mafanikio ya matibabu yatategemea na ikiwa maradhi haya yametambulika mapema. Maradhi haya yakitambulika katika awamu ya kwanza (Stage 1), uwezekano wa kuishi baada ya kutibiwa ni 90%. Ikiwa yatatambulika katika awamu ya tatu (stage 3), uwezekano wa mgonjwa kuishi na baada ya matibabu ni 50% pekee,” aeleza.

Kuhusu suala la ukosefu wa pesa, Dkt Ganda anasema kwamba shida hujitokeza tokea mwanzo. “Kwa kawaida uchunguzi wa seli(biopsy) unapofanywa, haulipii lakini ili kupokea matokeo, lazima ulipie,” anasema.

Kulingana na Dkt Ganda, wengi wa wakazi wa maeneo ya mashambani hawana pesa, ambapo kuna wale ambao hata baada ya kuja hospitalini na kufanyiwa biopsy, watashindwa kulipia, kumaanisha kwamba hawatapokea matokeo hayo.

Hii inamaanisha kwamba, kwa wale watakaopatikana na maradhi haya, hawatajua hali zao, na wataendelea kukaa nyumbani huku yakiendelea kuenea mwilini.

“Kisha kuna wale ambao hata licha ya kupokea matokeo yao, hawana uwezo wa kuendelea na matibabu.Watu wengi hawana kadi za bima ya afya ya NHIF. Na hata kwa wale walio nazo, kuna gharama zaidi wanazopaswa kushughulikia katika safari hii ya matibabu, pesa ambazo wengi hawana,” aeleza.

Kwa wale ambao hawana bima hii, asema, kibarua sasa huwa kusaka senti za kugharimia matibabu. “Matibabu ya kansa ya lango la uzazi yanaweza gharimu kati ya Sh300, 000 na Sh400, 000. Katika hospitali za kibinafsi, gharama zaweza fika hata Sh500, 000. Hiki ni kiasi kikubwa sana hasa kwa wakazi wengi wa mashambani,” aeleza.

Lakini pia Dkt Ganda anasema kwamba kuna changamoto ya hospitali na vituo vya afya katika maeneo ya mashambani kukosa vifaa, vile vile wahudumu waliofuzu kutambua na kudhibiti maradhi haya mapema.

Mwanzoni, anasema, katika harakati za kutambua maradhi haya, kuna uchunguzi sahili na nafuu unaofanywa wa Visual Inspection with Acetic Acid (VIA). Hii ni mbinu ya kutambua mapema na kukabiliana na baadhi ya ishara ambazo huenda zikaendelea kukua na baadaye kusababisha kansa ya lango la uzazi.

“Lakini tatizo ni kwamba baadhi ya hospitali hasa za mashambani hazina vifaa vinavyohitajika hapa, na pia wahudumu wao hawajapokea mafunzo ya kutumia mbinu hii na hata kukabiliana na ishara hizi mapema ili kudhibiti hali kabla ya mambo kuwa mabaya,” aongeza.

You can share this post!

Tanzania yakana mpango wa kufungia raia makwao kuepuka...

MARY WANGARI: Uwekezaji zaidi kisayansi na kiteknolojia...