• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Sonko atupwa ndani siku tatu

Sonko atupwa ndani siku tatu

Na RICHARD MUNGUTI

MASAIBU ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko Mbuvi Gidion Kioko yameongezeka baada ya  kusukumwa ndani hadi Feburuari 4, 2021 na kufunguliwa kesi mpya katika mahakama ya Kiambu Jumanne.

Umaarufu wa Sonko umeendelea kudidimia kila uchao huku akikumbwa na changamoto za kila aina.

Baada ya kushtakiwa katika mahakama ya Kiambu aliagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri kwa siku tatu kabla ya mahakama kuamua ikiwa itamnyima dhamana au la.

Kabla ya kukamatwa na kupelekwa mahakama hiyo iliyo kaunti ya Kiambu, Mahakama Kuu Jumatatu ilikataa kuzima hatua ya polisi kumsaka kumkamata na kumshtaki.

Kuandamwa huku kwa Sonko kunatokana na matamshi yake hivi punde kwamba yeye na maafisa wakuu serikalini wakiongozwa na katibu mkuu masuala ya usalama Dkt Karanja Kibicho walinunua magari makuu kuu na kuyateketeza moto 2017 ndipo chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kilaumiwe kwa vurumai hizo.

Mahakama ya Kiambu aliposhtakiwa Mike Sonko Februari 02, 2021. Picha/ Richard Munguti

Akihutubia hafla ya siasa hivi majuzi Sonko alitisha kutoboa siri jinsi uchaguzi mkuu wa 2017 ulivyoibwa na kunyima muungano wa Nasa ushindi.

Kufuatia matamshi hayo Dkt Kibicho aliandikisha taarifa katika makao makuu ya uchunguzi wa jinai na kumtaka Sonko afunguliwe mashtaka.

Sonko alikabiliwa na mashtaka sita ya kuongoza genge la watu kuvamia shamba la kibnafsi mtaani Buruburu kaunti ya Nairobi ambapo waliwapiga na kuwaumiza watu sita.

Gavana huyo alikanusha mashtaka hayo alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Kiambu Bi Stellah Atambo.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alipinga Gavana huyo anayesongwa na kesi kadhaa asiachiliwe kwa dhamana.

Ijapokuwa mawakili wake Sonko wakiongozwa na Dkt John Khaminwa waliomba mahakama imwachilie kwa dhamana DPP alipinga akisema atatoroka akiachiliwa kwa dhamana.

Stakabadhi ya mashtaka dhidi ya Mike Sonko . Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilielezwa Sonko aliwahi toroka gereza la Shimo la Tewa miaka ya hapo awali na kesi zinazomkabili zinaweza kuwa kishawishi chake kuchana mbuga.

Lakini hakimu alielezwa kuwa dhamana ni haki ya kila mshtakiwa hata kama anakabiliwa na kesi chungu nzima.

“Naomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana. Yuko nje kwa dhamana katika kesi zilizoko mahakama ya Milimani na hajakosa kufika kortini wakati wa kutajwa kwa kesi tatu zinazomkabili,” hakimu alielezwa.

Mahakama iliombwa isishawishiwe na midahalo mirefu ya DPP ya kuomba akatazwe dhamana. “Dhamana ni haki ya kila mshtakiwa hata kama anakabiliwa na shtaka lipi,” Bi Atambo alielezwa.

Stakabadhi ya mashtaka matano dhidi ya Mike Sonko. Picha/ Richard Munguti

Sonko alikanusha mashtaka kuwa mnamo Mei 25 2019 mtaani Buruburu Nairobi alivamia kwa nguvu na kinyume cha sheria shamba la kampuni ya Landmark International Property Limited.

DPP alisema shamba hilo ni nambari L.R Nairobi Block 78/8.

Mashtaka mengine yalikuwa mnamo siku hiyo ya Mei 25 2019 aliwaongoza watu alioandmana nao kuwapiga na kuwajeruhi Evans Obaga, George Chege, Paul Kahiga, Charles Karori na Joel Kinja Muturi.

Mashtaka yalidai Sonko aliongoza genge la watu kuvamia shamba hilo na kutekeleza uhalifu huo. “Nitatoa uamuzi iwapo utaachiliwa kwa dhamana mnamo Februari 4, 2021.”

You can share this post!

CECIL ODONGO: Raila asikate tamaa kuuza sera zake Mlima...

Mashirika yamlaumu DPP kwa kuondoa kesi dhidi ya polisi