• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Waigizaji wa Ukombozi Film wanavyonoa vipaji vya watoto Mombasa

Waigizaji wa Ukombozi Film wanavyonoa vipaji vya watoto Mombasa

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

NI kipindi cha mwaka mmoja na miezi minane pekee tangu kianzishwe, kikundi cha wasanii cha Ukombozi Film, Mombasa kimeanza kuonyesha mafanikio ya kutimiza malengo yao ya kuwakusanya watoto pamoja kwa madhumuni ya kutumia talanta zao kwa manufaa ya maisha yao.

Mwanzilishi wa kikundi hicho, Swaleh Nyuni amesema anafurahia kuona viongozi wa kikundi hicho wakiongozwa na Mwenyekiti, David Maraga wakiendelea kufanya juhudi za kuhakikisha wanachama wao wanazidi kuinua vipaji vyao vya sanaa ya uigizaji.

Katika mahojiano yaliyofanyika katika ukumbi wa Licodep katika mtaa wa Mount Sinai eneo la Likoni, Nyuni alisema kwa bidii inayotekelezwa na viongozi wa kundi hilo, ana uhakika litafika mbali na kutambulika kote nchini.

“Nina imani kubwa kama kikundi cha Ukombozi Film kitaendelea kuwika na kutoa wasanii wenye vipaji ambao wataweza kutambulika sio Mombasa, Pwani ama hapa nchini pekee bali hata huko ng’ambo,” mwanzilishi huyo aliambia Taifa Leo Dijitali.

Katibu wa kundi hilo, Mary Stella Baraza amesema kundi lake lina wanachama 30 wa makabila mbalimbali ambao wana malengo ya kudumisha umoja wao ili wafanikiwe kwenye malengo yao ya kuinua hali za maisha yao.

Wanachama wa kikundi cha Ukombozi Film ambacho kinafanya maozei katika ukumbi wa Licodep, mtaa wa Mount Sinai eneo la Likoni. Picha/Abdulrahman Sheriff

“Tumeamua kushirikiana na kupendana kama watu wa kabila na jamii moja kwa sababu tunatambua kuwa umoja ndio utakaotufikisha mbali kufanikiwa kwenye yale tunayotaka kuyatimiza,” akasema Mary.

Kinara Maraga amesema kwa kipindi kifupi tangu waanzishe kikundi hicho, wameona mwangaza wa mafanikio. “Kama hakukutokea janga la corona, tungelikuwa tumefika mbali zaidi,” akasema.

Nyuni anasema alikianzisha kikundi cha Ukombozi Film mnamo Aprili 2, mwaka 2019 ambapo kimewahi kutoa filamu mbili, moja ya ‘Mauko’ ambayo inaangazia zaidi juu ya mzazi mlezi kumlazimisha msichana kufanya naye tendo la ngono ili amnufaishe kifedha.

“Katika filamu hii, tunatoa ombi kwa wasichana wasikubali kunyanyaswa kimwili na walezi wao kwa sababu ya kutatuliwa matatizo yao. Tunaamini kama ni wajibu wa wazazi hao kuwalea kwa imani na kuwatimizia mahitaji yao bila ya kuwashurutisha kustarehe nao,” akasema Nyuni.

Filamu ya pili ya kikundi hicho inaitwa ‘Mkorogo’ iliyozinduliwa rasmi mwezi wa Agosti mwaka 2019 ambayo inawasihi wazazi hasa wazazi wa kike wasiwalazimishe kuwafungisha ndoa za mapema watoto wao wa kiume.

Mnamo mwaka uliopita na kabla ya janga la corona, Ukombozi Film ilizindua filamu mbili, moja ni ‘Upanga wa mapenzi’ unaozungumzia kusalitiana kwa mapenzi hali nyingine ni ‘Jopo la mahakama’ linaloonyesha hongo inavyomfanya maskini adhulumike anapotafuta haki yake.

Waigizaji wa kikundi cha Ukombozi Film wakitayarisha filamu zao nje ya ukumbi wa Licodep, eneo la Likoni. Picha/Abdulrahman Sheriff

Muigizaji mdogo wa kikundi hicho, Amina Rama aliye na umri wa miaka 10 anasema amekuwa akiwafurahisha wazazi wake kila anapofika nyumbani anapotoka kufanya mazoezi na waigizaji wa kikundi chake hicho cha Ukombozi.

“Huwa familia yangu inafurahika sana ninapofika nyumbani kutoka mazoezini na kuwaonyesha yale ambayo nimejifunza,” amesema Amina ambaye anaamini kwa msaada wa kikundi hicho atafika mbali katika sanaa hiyo ya uigizaji.

Naye Naomi Nyambaso anasema yeye na nduguye Meshack Nyambaso wanapofika nyumbani huwa wanawaonyesha watu wa kwao yale wamejifunza na hivyo wazazi wao wanafurahikiwa na kuwasihi kuendeleza vipaji vyao.

You can share this post!

Felly Mulumba kuisakatia Bandari wikendi

Olunga apimwa corona kujiandaa kwa Kombe la Dunia la Klabu