• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Mvua ya mabao Old Trafford

Mvua ya mabao Old Trafford

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United walisawazisha rekodi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kutinga mabao tisa katika mchuano, dhidi ya Southampton ambao walimaliza mchezo wakiwa wachezaji tisa pekee mnamo Jumanne usiku.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Southampton, almaarufu The Saints, kutoa ndani magoli tisa bila jibu katika muda wa miezi 16; baada ya kulishwa kichapo sawia na Leicester City mnamo Oktoba 2019.

Aidha, ni mara ya tatu pekee kwa timu kupoteza 9-0 kwenye ligi, United wakihusika tena katika kutoa kichapo kama hicho dhidi ya Ipswich Town mnamo 1995.

Katika mchuano huo wa Jumanne uwanjani Old Trafford, wageni walilishwa kadi nyekundu dakika ya pili ya mchezo na kuwapa United fursa nzuri ya kumimina mabao manne kabla kwenda mapumzikoni.

United hawakuwaonea huruma wapinzani wao katika kipindi cha pili huku wakipepeta magoli mengine matano katika dakika 21 za mwisho – japo kibarua chao kilikuwa mteremko zaidi baada ya mchezaji wa pili wa Saints kuuma kadi nyekundu mechi ikielekea tamati.

Kipenga cha mwisho kililia kiduchu tu kabla United kusawazisha rekodi yao ya klabu ya ushindi wa 10-0, uliopatikana dhidi ya Anderlecht ya Ufaransa mnamo 1956.

Mvua hiyo ya magoli ilifanya ushindi wao kuwa mtamu hata zaidi kwani tofauti yao ya mabao, 19, inazidiwa tu na ile ya viongozi wa ligi na watani wao Manchester City, walio na tofauti ya magoli 24.

United sasa wamekalia nafasi ya pili kwa alama 44 baada kusakata mechi 22, sawa na City ingawa wana mechi mbili za akiba.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na mabingwa watetezi Liverpool kwa alama 40 baada na mechi moja ya akiba dhidi ya United.

Leicester wanafunga nne-bora kwa alama 39 pia wakiwa na mechi moja ya akiba.

Kocha Ralph Hasenhuttl wa Southampton alisikitikia kichapo hicho cha 9-0 kutoka kwa United, akisema kinauma zaidi kuliko cha Leicester City.

“Tulicharazwa kwa njia ya kusikitisha. Inauma. Hali ni ile ile: mchezaji mmoja katolewa mapema katika mechi na kufanya dakika 90 zilizosalia kuwa mlima mgumu kupanda,” alisema Hasenhuttle baada ya mchuano.

“Nitachukulia matokeo haya kwa njia tofauti sababu tumekuwa tukipata matokeo mazuri, na tulitarajia kucheza vizuri. Ni kawaida timu kuchanganyikiwa wachezaji wao muhimu wanapotolewa. Ni matokeo ya kushangaza, mabao yaliingia kirahisi. Ni vigumu kueleza kichotokea, lakini itabidi tukubali. Hii haimaanishi tumekata tamaa, la. Tungali na muda wa kujirekebisha,” aliongeza.

Naye kocha Ole Gunnar Solskajaer alipongeza wachezaji wake kwa kufunga mabao mengi, mbali na kucheza vizuri.

“Tumesubiri kwa muda mrefu kuona washambuliaji wetu wakitinga mabao mengi kiasi hicho. Nilifurahia tamaa yao ya kutafuta mabao, na wengi wameonyesha dalili za kufanya vizuri zaidi siku za usoni.”

Waliofunga mabao ya United: Wan-Bissaka (18), Rashford (25), Bednarek (34, bao la kujifunga), Cavani (39 minutes), Martial (69 na 90), McTominay (71), Bruno Fernandes (87 penalti), James (90+3).

You can share this post!

Wazazi wa wanafunzi wanaoteketeza mabweni walipe gharama...

FAUSTINE NGILA: Vita vya Iran, Israel visizuie ukuaji wa...