• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
WANDERI KAMAU: Tukumbuke amani ni deni tutajilipia sisi wenyewe

WANDERI KAMAU: Tukumbuke amani ni deni tutajilipia sisi wenyewe

Na WANDERI KAMAU

KUFUATIA ghasia za kikabila zilizoshuhudiwa nchini kati ya 1991 na 1992, marehemu Daniel Moi aliteua tume maalum iliyoongozwa na Jaji Akilano Akiwumi kuchunguza chanzo kikuu cha machafuko hayo.

Jukumu jingine la tume hiyo lilikuwa kupendekeza hatua ambazo zingechukuliwa ili kuzuia ghasia zingine kutokea.

Ingawa tume ilimaliza uchunguzi huo na kumkabidhi Bw Moi ripoti yake, hilo kamwe halikuzima wimbi la ghasia za kikabila kuenea nchini.

Ilikuwa sawa na kuzima moto kwa tone la maji. Ghasia hizo zilitokea tena 1997 hasa katika eneo la Bonde la Ufa na baadhi ya maeneo ya Pwani.

Jamii mbalimbali ziligeukiana kwa tofauti za kisiasa. Zingine ziliona wenzao kama “wageni” na “wavamizi” waliostahili “kurejeshwa makwao” kwa vyovyote vile.

Nyumba zilichomwa. Mali ikaharibiwa. Maelfu wakaachwa bila makao. Mamia wakajeruhiwa huku wengine wakiuawa kikatili.

Ilikuwa ni taswira ya kutamausha sana. Wasiwasi ulitanda kote huku wanasiasa wakilaumiana kuhusu aliyesababisha mapigano hayo.

Serikali ya Bw Moi iliulaumu upinzani, nao upinzani ukamlaumu Rais na baadhi ya mawaziri wake kwa kufadhili mapigano hayo hususan katika Bonde la Ufa.

Juhudi za kupata jibu kuhusu kiini cha machafuko yaliyotokea ziligeuka kuwa mchezo wa kulaumiana. Kila aliyeelekezewa lawama alifanya awezavyo kujitakasa. Alijikosha dhidi ya kila tope alilorushiwa.

Wale wote waliotuhumiwa kushiriki kwenye ghasia hizo walibaki huru, nao walioathiriwa wakageuka wakimbizi na maskwota katika nchi yao wenyewe. Nchi waliyoifurahia na kuifaharikia iligeuka kuwa chemichemi ya majonzi na vilio visivyoisha.

Juhudi za kutafuta haki ziligeuka kuwa mchezo wa paka na panya. Hakuna idara iliyowajibika hata kidogo! Majaji na mahakimu waliwaondolea mashtaka washtakiwa kwa misingi ya “kukosa ushahidi.”

Wahasiriwa wakapoteza matumaini ya kupata haki. Wakawa wanaishi tu, maisha ya hofu na mashaka, maisha ya kubahatisha, maisha ya leo kesho wasijue itakuwa vipi.

Haya yote yalipokuwa yakiendelea, nchi zingine za Afrika zilikuwa katika utandu uo huo.

Rwanda ilikuwa ikijaribu kujijenga upya baada ya kukumbwa na mauaji ya kimbari mnamo 1994.

Uganda ilikuwa ikijaribu kumkabili kiongozi wa waasi wa Lords Resistance Army (LRA), Joseph Kony, huku DR Congo iking’ang’ana kuyakabili makundi ya wanamgambo.

Nchi hizo zikawa zinaangaliana tu pasiwe na hata mmoja wa kumsaidia mwenzake.

Juhudi za mashirika kama Muungano Huru wa Nchi za Afrika (OAU) na Umoja wa Mataifa (UN) hazikuzaa matunda hata kidogo.

Uhuru wa Afrika ulikuwa umegeuka kuwa giza kuu lililotanda kila mahali. Giza la mikosi na misukosuko. Je, Afrika ingejikomboa?

Uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia, mkosi ule ule wa chuki za kikabila umeanza kutunyemelea tena. Dalili za vita zimeanza kujitokeza, japo kwa umbali. Ni kama hatujasoma lolote.

Tumeanza kuwaona wenzetu kama “wageni” na “maadui” wabaya. Nani atatuondolea laana hii? Jawabu: tukumbuke amani ni deni tutakalojilipia sisi wenyewe!

[email protected]

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Mabunge ya kaunti yasiwe na pupa...

Arati, Osoro, Ng’eno na Sonko kuzimwa kuwania viti...