• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
Sonko aangua kilio kortini, adai kuna jaribio la kumuua

Sonko aangua kilio kortini, adai kuna jaribio la kumuua

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Sonko aliangua kilio kortini Jumatano wakati wa kusikizwa kwa kesi ya ufisadi wa Sh14 milioni dhidi yake baada ya mawakili waliokuwa wanamtetea kujiondoa.

Ilibidi Hakimu Mkuu Douglas Ogoti kumtuliza akimsihi aache kulia.

“Wacha kulia. Tulia kwanza Bw Sonko. Jipe nguvu ndipo ueleze mahakama vile unataka ikusaidie,” Bw Ogoti alimbebeleza.

“Naomba mahakama inipe muda nijiandae kwa vile mawakili Cecil Miller, George Kithi na wengine wamejiondoa katika kesi hii. Sina wakili wa kujitetea. Naomba siku 14 nijiandae na pia niwatafute mawakili wengine kuniwakilisha,” akasema Bw Sonko.

Alipokuwa akiendelea kulia, wakili John Khaminwa aliingia kortini na kuambia mahakama kuwa ameombwa kumwakilisha Bw Sonko katika kesi za ufisadi zinazomkabili akiwa na mawakili Assa Nyakundi na Wilson Nyamu.

Wakati huo huo, OCS wa kituo cha polisi cha Gigiri (OCS) aliamriwa ahakikishe usalama wa Bw Sonko.

Hii ni baada ya Bw Sonko kudai kuna mtu aliyejaribu kumdunga sindano ya sumu akiwa ndani ya seli usiku wa kuamkia Jumatano.

Hakimu Mkuu Ogoti pia alimwamuru OCS pamoja na afisa anayechunguza kesi dhidi ya Bw Sonko wasiwaruhusu watu kumwona isipokuwa watu wa familia yake, daktari na mawakili.

Mbali na agizo hilo, Bw Ogoti alimwamuru OCS amfikishe Bw Sonko katika mahakama ya Kiambu leo saa nane, wakati wa kuamuliwa ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana katika kesi aliyoshtakiwa ya kuvamia ardhi ya kampuni ya kibinafsi.

Pia alishtakiwa kwa kuwapiga watu na kuwaumiza wakati wa vurugu hiyo mnamo 2019 mtaani Buruburu, Nairobi.

Hakimu alisema usalama wa mshukiwa ni muhimu sana na kamwe hapasi kujihisi maisha yako hatarini akiwa na maafisa wa usalama. Akitoa agizo hilo Bw Ogoti alisema madai ya kuhatarishwa kwa maisha ya Bw Sonko ama mshukiwa yeyote yule hayapasi kuchukuliwa kijuujuu.

Mawakili wa Bw Sonko walikuwa wameomba azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga bada ya kuzuiliwa peke yake katika kituo cha Gigiri waliposema alilala kwenye sakafu bila gondoro.

Dkt Khaminwa alieleza mahakama kuwa mshtakiwa ni mgonjwa na anahitaji kutumia dawa za presha.

Dkt Khaminwa alisema usiku wa Feburuari 2, 2021 mtu aliyekuwa na sindano alijaribu kumdunga Bw Sonko lakini akapiga duru.

Awali Bw Sonko alilia mahakamani na kueleza alishtakiwa katika mahakama ya Kiambu kwa sababu alimtaja Bi Christine Pratt Kenyatta katika kesi ya uteuzi wa naibu wa gavana wa Nairob,i Bi Anne Kananu Mwenda.

Hakimu alimsihi Bw Sonko ajitulize.

ndipo awasilishe tetezi zake za kuomba apewe muda wa kuwateua mawakili wengine katika kesi ya ufisadi inayomkabili.

Bw Ogoti aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 10, 2021.

You can share this post!

Wanaonipuuza urais 2022 watashangaa – Joho

Mbio za Ras Al Khaimah zafutwa