• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Sonko hatarini kushtakiwa kwa madai ya ugaidi

Sonko hatarini kushtakiwa kwa madai ya ugaidi

Na RICHARD MUNGUTI

MASAIBU ya aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, yaliongezeka Jumatano ilipofichuka kuwa serikali inapanga kumshtaki kwa madai ya ugaidi.

Dakika chache tu baada ya kuondolewa katika mahakama ya kesi za ufisadi Milimani Nairobi, ambako anakabiliwa na kesi ya ufisadi wa Sh14 milioni, Sonko alipelekwa katika mahakama ya Kahawa, kaunti ya Kiambu.

Katika mahakama hiyo kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU) kiliomba kupewa siku 30 kuendelea kumzuilia kikichunguza madai ya ugaidi dhidi yake.

Mnamo Jumanne , Sonko alishtakiwa katika mahakama ya Kiambu kwa uvamizi wa shamba la kibinafsi jijini Nairobi, pamoja na kuwachapa watu sita.

Shtaka jipya la ugaidi linaongezea mahangaiko yanayomkabili Sonko ambaye aliondolewa madarakani mwezi Desemba mwaka jana.

Ombi la ATPU liliwasilishwa katika mahakama ya Kahawa inayoshughulikia kesi za ugaidi. Mahakama hii ilizinduliwa mnamo Desemba 11, 2020 na Jaji Mkuu aliyestaafu David Maraga.

Akiwasilisha ombi la kumzuilia Sonko kwa muda wa siku 30, Inspekta Newton M Thimangu, alisema anahitaji muda kukamilisha mahojiano na gavana huyu anayezongwa na masaibu tela.

Insp Thimangu aliomba hakimu wa Mahakama hiyo airatibishe kesi hiyo kuwa ya dharura. Pia aliomba mahakama itoe maagizo mengine inayoona yanafaa katika usakaji wa haki.

Insp Thimangu amefichua katika ushahidi aliowasilisha kortini kuwa Sonko anahusika na vitendo vya ugaidi.

“Taarifa za ujasusi nilizopokea zasema kuwa Sonko anawasajili wanamgambo wa kuvuruga amani na utangamano nchini,” asema Insp Thimangu katika afidaviti aliyowasilisha kortini.

Afisa huyo amesema kuwa kundi hilo la wanamgambo litaongoza machafuko nchini yatakayopelekea wananchi wapenda amani kuteseka bure.

Sonko, mahakama ilielezwa kuwa atafunguliwa mashtaka makali kwa mujibu wa sheria za ugaidi.

Afisa huyo mkuu wa uchunguzi wa jinai alieleza mahakama kuwa , Sonko yuko na ushawishi mkubwa na atavuruga juhudi zote za polisi za kupata ushahidi wanaotazamia kutoka kwake.

“Sonko yuko na ushawishi mkubwa na akiachiliwa kwa dhamana kwa sasa itakuwa vigumu kupokea ushahidi unaotakiwa,” asema Insp Thimangu.

Afisa huyo asema usalama wa nchi ni kigezo muhimu cha ustawi na kamwe wanaouvuruga wanatakiwa kuchukuliwa hatua. Hakimu mkuu Diana Mochache aliombwa akubalie ombi hilo na kuamuru Sonko azuiliwe kwa siku hizo 30.

You can share this post!

Mbio za Ras Al Khaimah zafutwa

Raila ajiondolea lawama Ruto kutengwa katika serikali ya...