Raila asema anaweza kuingia handisheki na Ruto

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga jana alieleza kuhusu uwezekano wake kubuni mwafaka wa kisiasa na Naibu Rais William Ruto kabla ya uchaguzi wa 2022.

Akihojiwa jana na kituo cha redio cha Inooro FM, Bw Odinga alisema hana tofauti zozote za kibinafsi kati yao, lakini huwa zinatokana na misimamo yao ya kisiasa.

“Sina tofauti za kibinafsi na Dkt Ruto. Huwa tu sipendezwi na namna ambavyo huwa anaendeleza siasa zake,” akasema Bw Odinga.

Wawili hao wamekuwa wakirushiana maneno makali, Dkt Ruto akimtaja Odinga kama “aliyevuruga mipango na utendakazi wa Jubilee” kufuatia handisheki kati yake na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa akijitenga na madai hayo, akisisitiza hakuna mwanachama wa ODM anayehudumu kama waziri serikalini.

Wakati huo huo, alieleza sikitiko lake kuhusu dalili za kuchipuka upya kwa ghasia za kisiasa, akisema Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) inapaswa kuwakabili wanasiasa wanaoeneza matamshi ya chuki bila kujali hadhi yao, wala mirengo ya kisiasa wanayoegemea.

Kwenye mahojiano hayo, Bw Odinga aliwaacha wafuasi wake gizani kuhusu ikiwa atawania urais mwaka ujao au la.Bw Odinga amekuwa akikwepa kueleza wazi ikiwa atawania nafasi hiyo, badala yake akisema atatangaza uamuzi wake baadaye.

Alisisitiza kuwa lengo lake kwanza ni kuhakikisha masuala yaliyojumuishwa kwenye ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) yamezafikiwa.

“Baada ya handisheki, tulikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta kutozungumzia lolote kuhusu 2022. Hadi sasa, sijui kama nitawania urais japo nitatangaza wakati mwafaka utakapofika,” akasema Bw Odinga.Kauli yake inaonekana kuendelea kuwakanganya wafuasi wake.

Kufikia sasa, wale ambao wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ni magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Hassan Joho (Mombasa).Licha ya kuwa katika mstari wa mbele kuendeleza ngoma ya BBI, Bw Odinga alisema anafanya hivyo kulingana na mwafaka waliofikiana na Rais Kenyatta.

“Tulikubaliana na Rais Kenyatta aendeleze ajenda za serikali huku nikivumisha ngoma ya BBI,” akasema.

Habari zinazohusiana na hii

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki

Watamjaribu Baba?