• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Wewe si ‘hasla’, ulikuwa karibu na Mzee Moi hata kuliko Gideon Moi, Kalonzo amwambia Ruto

Wewe si ‘hasla’, ulikuwa karibu na Mzee Moi hata kuliko Gideon Moi, Kalonzo amwambia Ruto

Na SAMMY WAWERU

Kiongozi wa chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka amemsuta Naibu wa Rais William Ruto kuhusu kauli yake ya ‘hasla’.

Makamu huyo wa zamani wa Rais amesema kutokana na jinsi Bw Ruto aliinuliwa na Rais Mstaafu, Mzee Daniel Arap Moi (ambaye kwa sasa ni marehemu) wakati akiwa Rais, hapaswi kujiweka katika kiwango cha mahasla – nembo ambayo Naibu wa Rais amekuwa akitumia kufanya kampeni kuingia Ikulu 2022 akidai ni mchakato wa kuinua walala hoi.

Bw Kalonzo alisema hayo mnamo Alhamisi katika hafla ya ukumbusho wa Mzee Moi, mwaka mmoja baada ya kufariki. Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi pia walihudhuria ukumbusho huo wa Mzee Moi.

Kulingana na Kalonzo, Dkt Ruto ni mwanasiasa ambaye alikuwa karibu sana na Rais Moi wakati akiwa mamlakani.

“Inashangaza kuona ukiendesha siasa potovu kati ya nasaba zilizowahi kuwa mamlakani na walalahoi. Ulikuwa kijana wa karibu wa Mzee Moi, hata kuliko Gedion Moi,” akasema, akielekezea Naibu Rais matamshi hayo.

Bw Kalonzo alisema joto la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa nchini, linachangiwa na baadhi ya wanasiasa wanaoendesha siasa potovu.

Akirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo wabunge wawili waliangushiana makonde hadharani katika hafla ya mazishi, Kalonzo amemlaumu Naibu Rais kwa kile amedai “amegeuza na kuteka mawazo ya wanasiasa wanaoendelea kumfanyia kampeni”.

Mapema juma hili, mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro na mwenzake wa Dagoretti, Simba Arati walitwangana katika mazishi ya babake naibu gavana wa Kisii Joash Maangi, Mzee Abel Gongera.

Naibu wa Rais Dkt Ruto na kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga walihudhuria hafla hiyo ya mazishi.

You can share this post!

Wabunge waachwa vinywa wazi kuambiwa Sh6.2 bilioni za...

Dkt Mutua awataka wanasiasa kuheshimu familia za waliofiwa