Raila ajiondolea lawama Ruto kutengwa katika serikali ya Jubilee

Na SAMMY WAWERU

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amejiondolea lawama kwamba amechangia Naibu wa Rais William Ruto kutengwa katika utawala wa serikali ya Jubilee.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakilalamikia Naibu Rais kutengwa katika maamuzi ya serikali, wakinyooshea Bw Odinga kidole cha lawama.

Baada ya salamu za maridhiano, maarufu kama Handisheki, mnamo Machi 2018 kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, Ruto hajakuwa akishikirishwa katika baadhi ya mikakati ya serikali ya Jubilee.

Bw Odinga amekuwa katika mstari wa mbele ‘kunadi sera za serikali’, huku Rais akimpa mamlaka kuzindua miradi ya maendeleo.

Akimsuta Naibu wa Rais, kinara huyo wa upinzani Alhamisi alisema Dkt Ruto amekuwa akishiriki kampeni kutafuta kura kuingia Ikulu 2022 badala ya kumsaidia Rais Kenyatta kuafikia ajenda za Jubilee.

“Makamu wa Rais na kikosi chake wamemuacha Rais afanye kazi peke yake. Alianza kampeni 2017. Anapodai Handisheki na ODM imezuia kazi kuendelea inashangaza, Rais mwenyewe anaonekana kufanya kazi,” Bw Odinga akasema.

Dkt Ruto amekuwa akidai tangu Rais na Bw Odinga waamkuane kupitia salamu za maridhiano, malengo ya serikali ya Jubilee yamekwama.

Kulingana na Odinga, Naibu Rais anapaswa kuwajibikia utendakazi mbaya wa serikali ya Jubilee tangu iingie mamlakani 2013.

“Sasa anaongea kuhusu toroli…Anapotosha Wakenya, amesahau ahadi za tarakilishi kwa wanafunzi alizotoa kwa Wakenya, kubuni nafasi milioni moja za kazi kwa vijana kila mwaka na kujenga viwanja vya kisasa katika kila kaunti,” Bw Odinga akasema, akimsuta Dkt Ruto kwa kauli yake ya ‘hastla’.

Licha ya wawili hao katika siku za hivi karibuni kuonekana kutofautiana vikali na kurushiana maneno mazito hadharani, Raila alisema hawana uhasimu wowote kati yao.

Alisema hayo katika mahojiano ya pamoja na kituo cha redio cha Inooro na runinga, vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

Alipoulizwa endapo yuko tayari kufanya salamu za maridhiano kati yake na Ruto alijibu: “Sihitaji handisheki nyingine kwa sasa, tuafikie iliyopo kwanza.”

Habari zinazohusiana na hii

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto