• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
MARION MAPENZI: Naipenda sana Barca, lengo ni kucheza soka ya kulipwa ughaibuni

MARION MAPENZI: Naipenda sana Barca, lengo ni kucheza soka ya kulipwa ughaibuni

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KILA mwanasoka wa pande zetu huku Kenya, Afrika Mashariki na sehemu nyingine zote barani Afrika huwa wanapenda kubandikwa jina la mchezaji aliye maarufu duniani.

Marion Mapenzi Chengo, nahodha wa Ukunda Starlets FC anajivunia kuitwa jina la aliyekuwa mchezaji wa timu anayoipenda ya Manchester United ya England, Wyne Rooney japo yeye anacheza soka ya wanawake.

Marion alipewa jina hilo la Rooney kwao nyumbani Kilifi ambapo ndipo kuna familia yake, jina ambalo linazidi kumpa moyo mkubwa wa kuinua kipaji cha uchezaji wake akidhamiria kufikia kiwango cha kucheza soka la kulipwa ng’ambo.

“Ninapoitwa Rooney, huwa nasikia raha na inanipa moyo mkubwa wa kuongeza bidii ikatika mazoezi nikitia nia ya kuinua kipaji cha uchezaji wangu ufikie ule utakaonipa uwezo wa kusajiliwa na mojawapo ya klabu maarufu barani Ulaya,” amesema Marion.

Ingawa Marion aliye na umri wa miaka 19 anajivunia kuitwa Rooney na mashabiki wa soka wa Kilifi, anasema binafsi anaipenda zaidi timu ya Barcelona FC ya nchini Uhispania na angelipendelea kilele cha uchezaji wake aichezee Barcelona Ladies.

“Kiuhakika naipenda zaidi Barcelona lakini Manchester United naipenda kidogo kwa sababu nimepewa jina la mchezaji wao wa zamani Rooney,” msichana huyo mwanafunzi wa kidato cha tatu aliambia Taifa Leo Dijitali.

Chipukizi Marion Mapenzi. PICHA/ ABDULRAHMAN SHERIFF

Marion anahadithia kuwa alianza kupenda soka akiwa darasa la nne katika shule ya Madamani Primary mnamo mwaka 2017 alipoamua kuitosa katika mchezo huo ikiwa ni njia mojawapo ya kujiepusha kujiingiza katika anasa na utumizi wa mihadharati ambazo zingemuharibia maisha.

“Nilifurahika mwaka huo kwani nilifanikiwa kuwa mmoja wa wachezaji waliochaguliwa kuwakilisha timu ya mseto ya Pwani kwenye mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi ya Kitaifa yaliyofanyika Meru,” akasema Marion aliyejiunga na shule ya Kilifi Mixed Secondary.

Mwanasoka huyo aliyekuwa akisoma shule ya Migori Education Centre huko jimbo la Nyanza alifika mjini Ukunda kwa kaka yake mnamo mwaka 2019 na kuona wasichana wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa Nacet na wakamkubalia ajiunge nao.

“Ni wakati huo ndipo nilifurahikia na nikamuomba Mkurugenzi wa Ufundi Martin Wekesa aliyenikubali nijiunge na timu yake ya Ukunda Starlets ambayo mpaka sasa ndiyo ninayoichezea,” akasema.

Marion amemshukuru Wekesa kwa kumpa fursa ya kuinua kipaji cha uchezaji wake katika timu hiyo ya Ukunda Starlets ambapo hivi sasa ndiye anayeshikilia wadhifa wa unahodha, cheo ambacho anakichukulia kuwa muhimu chenye jukumu la kuwaunganisha wanasoka wenzake.

“Nikiwa nahodha wa timu yetu hii, ninashirikiana vizuri na wachezaji wenzangu tukiwa na lengo moja la kuipeleka mbali timu yetu na nina matumaini makubwa ya kuhakikisha tunadumisha umoja kati yetu ili tupate kuinua vipaji vya uchezaji wetu,” akasema.

Marion amepania kuhakikisha anakuwa mchezaji wa kutajika akilenga zaidi kuvutia maskauti wa ng’ambo pamoja na wale wanaohusika kwa uteuzi wa wachezaji wa kujiunga na timu ya taifa ya soka la wanawake ya Harambee Starlets.

“Nina lengo ambalo nataka nilifikie wakati huu la kutambuliwa kuchezea timu ya Harambee Starlets kwani ni kutokana kuonekana hapo, inakuwa rahisi kwa mchezaji kuvutia maajenti na maskauti wa kukufikiria kweneda kufanya majaribio na klabu za ng’ambo,” akasema.

Kwake Marion anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji anasema ana nia kufikia kiwango walichofikia wanasoka wengine wa Pwani kina Elizabeth Katungwa anayechezea soka la kulipwa Ulaya na Mwanahalima Adam ambaye ni straika wa kuaminika wa timu ya taifa.

“Nina hamu kubwa na nafanya bidii nifikie viwango vya wachezaji hao ili name nitambulike na niweze kufikia lengo langu la kuwa mchezaji wa kulipwa huko Ulaya na hasa nikipata fursa ya kujiunga na Barcelona Ladies,” akasema Marion.

You can share this post!

Raila ajiondolea lawama Ruto kutengwa katika serikali ya...

Ulinzi Stars kutumia uwanja mbadala Afraha Stadium...