• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Gor Mahia kusajili wanasoka wawili zaidi wa kigeni

Gor Mahia kusajili wanasoka wawili zaidi wa kigeni

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 19 na washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Kenya, wamemsajili upya beki na nahodha wao wa zamani, Harun Shakava aliyetamatisha mkataba wake na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Zambia (ZSL), Nkana FC, mwishoni mwa Januari baada ya kuwachezea kwa mwaka mmoja na nusu.

Naibu Mwenyekiti wa Gor Mahia, Francis Wasuna, amesema kurejea kwa Shakava aliyeagana nao mnamo Agosti 2019 kutapiga jeki safu yao ya ulinzi ambayo ilitepetea pakubwa baada ya kuondoka kwa Joash Onyango aliyeyoyomea Tanzania kuvalia jezi za Simba SC mnamo Agosti 2020.

Baada ya kufungwa jumla ya mabao 10 kutoka kwa APR ya Rwanda na CR Belouizdad ya Algeria kwenye kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League), Gor Mahia wamepachikwa pia magoli 10 kutokana na mechi nane zilizopita za FKFPL msimu huu.

Shakava anakuwa mchezaji wa tano wa haiba kuagana na Nkana chini ya kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na uchechefu wa fedha. Wanasoka wengine ambao wamebanduka kambini mwa miamba hao ni Idris Mbombo (DR Congo), Kelvin Mubanga, Allan Chibwe (Zambia) na nahodha wa zamani wa AFC Leopards, Duncan Otieno aliyetua Lusaka Dynamos ya Zambia. Kiungo wa zamani wa Kariobangi Sharks, Duke Abuya, pia yuko pua na mdomo kuondoa Nkana FC.

Chini ya kocha Carlos Manuel Vaz Pinto, Gor Mahia walifungua shughuli za kusajili wanasoka wapya katika muhula huu mfupi wa uhamisho kwa kujinasia huduma za fowadi raia wa Brazil, Wilson Fonseca kutoka Fortaleza FC nchini Brazil.

“Shakava ametia saini kandarasi ya miaka mitatu. Kocha alitaka wachezaji wanne zaidi baada ya kuteua watano atakaowatema muhula huu. Sasa tuna wanasoka wawili raia wa kigeni watakaowasili nchini wikendi hii,” akasema Wasuna katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Shakava alijiunga na Gor Mahia mnamo 2014 baada ya kuondoka Kakamega Homeboyz na akaongoza Gor Mahia kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu ya Kenya. Hata hivyo, atalazimika kusubiri zaidi kabla ya kuchezea miamba hao kwenye soka ya Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup).

“Hajaidhinishwa kutuchezea kwenye mikondo miwili ya mchujo dhidi ya Napsa. Hata hivyo, tutamsajili atuchezee katika gozi hilo la CAF baada ya kikosi kufuzu kwa hatua ya makundi,” akaongeza Wasuna.

Gor Mahia almaarufu K’Ogalo watakuwa wenyeji wa mkondo wa kwanza dhidi ya Napsa Stars jijini Nairobi mnamo Februari 14 kabla ya mchuano wa mkondo wa pili kuandaliwa jijini Lusaka mnamo Februari 21.

Shakava ambaye huenda akachezeshwa dhidi ya AFC Leopards katika FKFPL wikendi hii ugani MISC Kasarani, alipokezwa ukapteni wa Gor Mahia mnamo 2018 baada ya kuaminiwa kuwa kizibo cha beki wa Harambee Stars, Musa Mohammed, aliyetua Albania kuchezea FK Tirana. Musa kwa sasa anavalia jezi za Difaa El Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco.

You can share this post!

Otieno arejea kutoka Zambia kuwa kizibo cha Asieche kambini...

KRU yasema vikosi viko tayari kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup