• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
Shujaa, Lionesses wapata motisha ya Sh2.8 milioni kuenda Uhispania

Shujaa, Lionesses wapata motisha ya Sh2.8 milioni kuenda Uhispania

Na GEOFFREY ANENE

KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOC-K) imepiga jeki timu za taifa za Shujaa na Lionesses kwa maandalizi ya Olimpiki 2020 kwa Sh2.8 milioni Alhamisi.

Kaimu Katibu wa NOC-K Francis Mutuku alitoa hundi ya fedha hizo kwa wawakilishi wa wachezaji Janet Okelo na Sheila Chajira mbele ya maafisa wa Shirikisho la Raga Kenya (KRU) Joshua Aroni (Mwekahazina) na Thomas Odundo (Afisa Mkuu Mtendaji).

Kwa mujibu wa NOC-K, usaidizi huo utatumika katika usafiri wa timu hizo nchini Uhispania kwa mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande jijini Madrid ambayo yatajumuisha timu 12 katika vitengo vyote viwili.

Raga ni mojawapo ya michezo iliyochukua muda mrefu kuidhinishwa kurejea baada ya shughuli zote za kimichezo kusimamishwa kwa ghafla Machi 2020. Michezo nchini Kenya ilianza kurejea Septemba mwisho mwaka jana chini ya masharti ya afya ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, ingawa timu za taifa za raga zilipata idhini Novemba.

KRU ilifanya mipango ya mapema kuandaa vikosi hivyo kabla ya maandalizi rasmi ya Olimpiki kuanza.

“Usaidizi tunaotoa kwa timu zetu za raga ni mdogo kwa hivyo tunatumai serikali pia itajitolea kusaidia timu zitakazoenda Olimpiki haraka iwezekanavyo,” alisema Mutuku.

Aroni alishukuru NOC-K kwa mchango wake. “Tunashukuru NOC-K kwa kujitolea kwake kuhakikisha timu zinazoenda kushiriki Olimpiki mjini Tokyo zimejiandaa vizuri. Tutatumia msaada huu wa NOC-K kusaidia timu zetu kuenda Uhispania,” alisema afisa huyo na kufichua kuwa vikosi vya Kenya vitakavyoshiriki Madrid Sevens na mazoezi ya hali ya juu, vitatajwa Ijumaa.

“Tumejitahidi kufuata masharti ya afya ya ugonjwa wa covid-19. Kuandaa vikosi vyetu vizuri zaidi tulihitaji raslimali. Wadhamini wetu walijiondoa kwa sababu ya changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na janga hili. Usaidizi wa NOC-K utatusaidia, ingawa bado tunaomba wadhamini zaidi wajitokeze na kusaidia ili timu ziweze kufikia mahali pa kufanya bora zaidi,” aliongeza Aroni.

Nyota wa Lionesses, Okelo, alisema timu hiyo imekuwa ikitumia muda wake vizuri mazoezini na imezoea sasa kufanya mazoezi chini ya masharti ya covid-19, ingawa si rahisi. Alisema usaidizi mdogo unaopatikana unaweza kusaidia ratiba ya timu kufanya mazoezi.

You can share this post!

Ni mashabiki 40 pekee wataruhusiwa kushuhudia mechi

BBI: Karua atawezana?