• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Django FC inavyokuza talanta za chipukizi wa Uthiru

Django FC inavyokuza talanta za chipukizi wa Uthiru

NA PATRICK KILAVUKA

Lisilobudi hutendewa! Hiyo ndiyo kauli walioichukua na kuiaminia wadau wa timu ya Django FC inayopiga hema la mazoezi uwanja wa Shule ya Msingi ha Uthiru, kaunti ndogo ya Kabete kustawisha jahazi la timu hii kuvinusuru na kuvifinyanga vipaji vya vijana na kuwatandikia zulia la kutandizia boli, pamoja na kujimarisha kiafya na kimaisha.

Chini ya wanabenchi Charles Thiongo, kocha Dennis Waweru na mshirikishi Josphat Kamau wa timu, ilingoa nanga mwaka 2019 na wachezaji kumi na mbili ambao waliamua kila kitu huanza kwa hatua moja.

Timu meneja Thiongo alisema kwamba, licha ufadhili kuwa kikwazo mwanzoni, walijikasa kisabuni kuwaleta pamoja wanasoka hawa na nia ya kuona ndoto zao zitatimia.

“Wanasoka hawa walionyesha utajiri wa vipawa wakati walikuwa wanazichezea shule mbalimbali. Tulichukua hatua sasa ya kuona umaana wa kuvichongachonga vipawa vyao na sasa hivi vimewapa fursa nzuri ya kusakata boli,” akasema meneja Thiongo ambaye amehakikisha timu inatanuka zaidi na hata inashiriki katika vipute na ligi ya kaunti ndogo ya Kabete, Kiambu.

Naye kocha Waweru anadokeza kwamba, ukufunzi wake hakuanza tu na timu hii bali ni kipaji adimu ambacho alianza kukichochea kama angali shuleni. Amewahi kuwa kocha wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Thika alikosomea akiwa bado mwanagenzi kabla kuguria ile ya Wavulana ya Muranga na kuwa naibu kocha.

Kikosi cha Django FC kutoka Uthiru kikicheza dhidi ya Sodom FC uwanjani Kihumbuini, Kangemi. Picha/Patrick Kilavuka

Anasema kile ambacho kilimvutia kuwa kocha ni kwamba, akiwa bado shuleni alikuwa anapenda sana kuwahimiza wachezaji wa kabumbu kwa kuwapigia kelele za kuwasabikia na kufuatilia kwa makini mawaidha ya kocha wao.

“Nilikuwa pia mshauri mkuu wa wachezaji japo mimi si kuwa mchezaji. Ila, mawaidha yangu wakati yalipokuwa yanatiliwa maanani, timu ilikuwa inafanya vyema kwenye mashindano ya shule za upili hadi tukawa tunavuma,” asema kocha huyo ambaye ameiongoza timu hii tangu iasisiwe.

Anakariri kwamba, kutizama michezo ya ughaibuini hususa ya Uingereza na vile makocha wanavyoonyesha weledi wao, alipata kujifunza mawili matatu na yote tisa, kumi amekuwa sasa mkufunzi ambaye anaweza kupanua timu kupitia vinganganyiro vikiwemo kile cha Kabete Self Sponsored na Ligi ya Shirikisho la Kandanda, Kabete.

Katika kipute cha Kabete Self Sponsored, mwaka 2020 ambacho kilisitishwa kufuatia mkurupuko wa Corona japo kimeendelezwa mwaka huu, ilifika katika awamu ya makundi na akakamata namba tatu, nyuma ya Gitaru United na Gitaru Tiger.

Imeshiriki pia katika kipute cha Westlands Soccer Association na kuondolewa katika kiwango cha makundi. Fauka na kushiriki katika makala ya saba ya Tim Wanyonyi Super Cup, 2020 na kubanduliwa katika mkundo wa makundi katika Wadi ya Mt View.

Kuimarika kwa timu kumetokana na msingi mwema wa mwamba usiokuwa kitabaka, inajiondolea ubutu kwa kufanya mazoezi kuanza jumatatu hadi Ijumaa kabla kujibwaga uwanjani wikendi kucheza mechi za kirafiki au Vipute, wazazi na mashabiki kuikumbatia na kutambishwa kwa ushauri nasaha kwa wachezaji. Pia, wachezaji wanahimizwa kutumia mtandao wa Youtube kujizolea maarifa zaidi mbali na kuitizama michuano ya soka ya Uingereza.

Kikosi cha Django FC kutoka Uthiru, Kaunti Ndogo ya Kabete kikipokea mawaidha kutoka kwa kocha Dennis Waweru kilipokuwa kikicheza dhidi ya Sodom FC uwanjani Kihumbuini, Kangemi.Picha/Patrick Kilavuka

Katika ya michuano ya kujinoa zaidi ambayo imepiga ni dhidi ya Sparks FC na kuizima 5-0, Royal Soccer Academy na kuambilia sare ya 1-1 na Sodom FC na kuagana sare ya 1-1.

Wanaomba wahisani zaidi kujitokeza kuisaidia kusukuma gurudumu ambalo limenuia kuipeleka katika hatua zaidi ya kusaidia wachezaji hawa.

Kikosi ni Kelvin Kinyanjui, John Kimani, Kelvin Wairati, Collins Maloba, Ephrahim Muriuki, George Mwangi, Brian Orina, John Kamau, Nicholas Malombe, Stephen Gaucho, Cornelius Mulwa, Francis Lugaka, Moffat Kazungu, Moses Odhiambo, Samuel Kariuki, Amos Kelly miongoni mwa wengine.

You can share this post!

LAMU: Gavana Twaha ajiteua kuhudumu kama waziri

Wasiwasi Ghana wabunge 15 wakiugua corona