• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Kenya iliporwa Sh330.5 milioni ikipoteza pia uenyeji wa Dimba la CHAN 2018

Kenya iliporwa Sh330.5 milioni ikipoteza pia uenyeji wa Dimba la CHAN 2018

Na DAVID MWERE

SERIKALI imeshindwa kupata wamiliki wa kampuni ya Auditel Engineering & Services Limited ambao walitoweka na Sh330.5 millioni baada ya kulipwa na Wizara ya Michezo kuweka vifaa vya usalama katika viwanja mbalimbali kote nchini kwa Dimba la CHAN 2018.

Hapo Februari 4, Kirimi Kaberia, ambaye fedha hizo zililipwa kwa njia ya utata wakati akihudumu kama Katibu wa Wizara ya Michezo, alithibitisha mbele ya kamati ya bunge kuwa kampuni hiyo haikufanya kazi ambayo ilikuwa imepewa licha ya kupokea mamilioni hayo.

Alieleza Kamati ya Bunge kuhusu uhasibu (PAC) kuwa kampuni hiyo ilitoweka mara tu ililipwa fedha hizo.

“Sijui hatima ya Auditel,” Kaberia aliambia kamati hiyo chini ya Mbunge wa Ugunja, Opiyo Wandayi.

Kamati hiyo inakagua akaunti za kifedha za wizara hiyo za kipindi cha 2017/2018. Kaberia alikuwa na kibarua kigumu kueleza kwanini wizara hiyo ililipa fedha kabla ya kazi kufanyika.

Maelezo kuwa kampuni hiyo ilikuwa imependekezwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na kuwa serikali haikuwa na njia nyingine, bali kufuata masharti ya CAF, hayakupokelewa vyema na kamati hiyo.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilisema kuwa Auditel ilisaini kandarasi ya Sh1.61 bilioni na wizara hiyo mnamo Septemba 14, 2017, kuweka vifaa vya usalama katika viwanja mbalimbali kote Kenya.

Shughuli hiyo ilifaa kufanywa kabla ya Kombe la Bara Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka katika mataifa yao almaarufu CHAN mwaka 2018.

Dimba hilo lilifaa kufanyika Kenya mwaka 2018, lakini likahamishiwa Morocco baada ya Kenya kuchelewa katika kuweka vifaa vinavyofaa tayari.

Utoaji wa kandarasi hiyo, ambao pia kwa mujibu wa Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unazingirwa na utata, ulifaa kutekelezwa katika kipindi cha miezi minne.

Kandarasi hiyo ilikuwa ya kubadilisha sura ya viwanja vitano – Jomo Kenyatta (Machakos), Moi Kinoru (Meru), Kipchoge Keino (Eldoret), Nyayo na Kasarani (Nairobi) – pamoja viwanja 10 vya kufanyia mazoezi vilivyotengewa mashindano hayo ya CHAN.

Kampuni hiyo ilipokea malipo ya kwanza ya asilimia 20 ikitumia hakikisho ya kiusalama kutoka kwa benki moja jijini Madrid nchini Uhipania mnamo Oktoba 30, 2017.

Ripoti hiyo ya ukaguzi inaonyesha kuwa dhamana hiyo ilikuwa halali hadi Februari 28, 2018 na kwa hivyo ilipitwa na wakati ukaguzi ulipokuwa ukifanywa Novemba 2018 na hakuna ushahidi kuwa ilihalalishwa tena.

Ushahidi huu ni wa wazi kuwa serikali huenda isipate tena fedha ilizolipa.

Hapo Alhamisi, Wandayi na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, ambaye anahudumu katika kamati ya PAC, walipigwa na butwaa kuwa kufikia wakati Kaberia alithibitisha kupotea kwa fedha hizo, hakuna uchunguzi ulikuwa umefanywa kutafuta wamiliki wa kampuni hiyo.

“Auditel ilipokea tu fedha na kupotea. Hii inaonekana kuwa njama iliyopangwa kuibia umma fedha. Ilipotelea wapi,” Wandayi alishangaa.

“Je, unafahamu kama kuna uchunguzi wowote unaendelea kuhusu Auditel?” Wandayi aliuliza Kaberi ambaye alijibu kuwa hakuna.

Duale alikerwa. “Unafahamu kuwa Auditel ilikuwa na ofisi mtaani Lavington na Westlands, lakini kwa ghafla, na baada ya kulipwa, imepotea na haiwezi ‘kupatikana’? Mbona hukuitisha mali ya kampuni hiyo itumiwe kama dhamana?” aliuliza Duale.

“Kama kamati, hatukuweza kuthibitisha kama kampuni hiyo bado ipo ama haipo kwa sababu hatukuweza hata kuwapata wafike mbele ya kamati hii,” alisema Duale.

Katibu wa sasa wa michezo Joe Okudo, ambaye alikuwa ameandamana na Kaberia aliambia kamati hiyo kuwa mara tu alichukua hatamu Februari 2020, wanaume wawili wa kizungu waliodai kuwa wamiliki wa Auditel, walifika katika afisi yake na kuitisha malipo mengine.

“Wanaume wengine wawili wa kizungu walikuja afisini mwangu kabla tu ya mkurupuko wa ugonjwa wa covid-19 mwaka jana wakitaka fedha zaidi. Kufikia wakati huo, hakuna kilichokuwa kimefanywa katika viwanja hivyo. Niliwaeleza nahitaji ushauri wa Mwanasheria Mkuu kuhusu ombi lao,” Okudo alieleza kamati hiyo.

“Hawakuwahi kurudi kwangu na pengine waliniona kuwa adui wao,” aliongeza.

Alipoulizwa na Duale iwapo alikuwa na uhakika wanaume hao wawili aliotaja walikuwa wamiliki wa Auditel, alisema, “Sikuwa na sababu ya kuwashuku kwa sababu walionekana kama wamiliki kamili.” – Imetafsiriwa na Geoffrey Anene

You can share this post!

Ighalo apata hifadhi Saudia

Real kumwajiri Allegri iwapo Zidane ataondoka