• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Ghost ataja 28 kuanza maandalizi ya Harambee Stars ya AFCON 2022

Ghost ataja 28 kuanza maandalizi ya Harambee Stars ya AFCON 2022

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Jacob “Ghost” Mulee ametaja kikosi cha wachezaji 28 wanaosakata soka humu nchini kwa ajili ya mechi za kufa-kupona za kufuzu kushiriki Kombe la Bara Afrika (AFCON) 2022 dhidi ya Mirsi na Togo zitakazofanyika mwezi ujao.

Katika kikosi chake ambacho kinahitaji ushindi mkubwa katika mechi zote na mojawapo kati ya Misri na Comoros zipoteze michuano yao miwili iliyobaki ndiposa Harambee Stars iiingie AFCON2022, Mulee amejumuisha washambuliaji Erick Kapaito (Kariobangi Sharks) na Elvis Rupia (AFC Leopards) wanaofukuzana vilivyo katika ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya 2021.

Kapaito amechana nyavu mara 12 naye Rupia yuko mabao mawili nyuma kutokana na mechi 10 na nane mtawalia. Mshambuliaji wa Gor Mahia Benson Omalla, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Kisumu Day, pia amejumuishwa katika kikosi hicho.

Kipa wa KCB Joseph Okoth, kiungo wa AFC Leopards Collins Shichenje na beki wa KCB Nahashon Alembi ni baadhi ya sura mpya katika kikosi cha Mulee ambacho kinakaribisha kiungo wa Wazito Kevin Kimani,31, aliyechezea Kenya mara ya mwisho mwaka 2015.

Mshambuliaji wa Tusker FC Henry Meja, ambaye alichezea timu ya taifa ya Under-20 almaarufu Rising Stars katika mashindano ya Cecafa mwaka 2020, pia ameitwa katika kikosi hicho kitakachoaanza mazoezi jijini Nairobi mnamo Februari 8.

Stars, ambayo inakamata nafasi ya tatu kwa alama tatu katika Kundi G, itaalika Mafirauni hapo Machi 22 kabla ya kuelekea Togo mnamo Machi 30. Misri inaongoza kundi hilo kwa alama nane. Inafuatiwa na wanavisiwa wa Comoros, ambao pia wamezoa alama nane lakini wanazidiwa kwa tofauti ya ubora wa magoli. Togo inavuta mkia kwa alama moja. Ghost hajazungumzia wachezaji wanaocheza nje ya Kenya, ingawa huenda wakajumuishwa baadaye.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa – Brian Bwire (Kariobangi Sharks), James Saruni (Ulinzi Stars), Joseph Okoth (KCB), Peter Odhiambo (Wazito);

Mabeki – Johnstone Omurwa (Wazito), Michael Kibwage (Sofapaka), Samuel Olwande (Kariobangi Sharks), Nahashon Alembi (KCB), Bonface Onyango (Kariobangi Sharks), David Owino (KCB), Daniel Sakari (Kariobangi Sharks), Baraka Badi (KCB);

Viungo – Lawrence Juma (Sofapaka), Kenneth Muguna (Gor Mahia), Collins Shichenje (AFC Leopards), Micheal Mutinda (KCB), Musa Masika (Wazito), John Macharia (Gor Mahia), Reagan Otieno (KCB), James Mazembe (Kariobangi Sharks), Oliver Maloba (Nairobi City Stars), Bonface Muchiri (Tusker), Kevin Kimani (Wazito), Abdalla Hassan (Bandari);

Washambuliaji – Erick Kapaito (Kariobangi Sharks), Elvis Rupia (AFC Leopards), Henry Meja (Tusker), Benson Omalla (Gor Mahia). 

You can share this post!

Kipa wa Ajax apigwa marufuku ya mwaka mmoja kwa kutumia...

Koma kulia, pambana kama mwanamume, hakimu amwambia Sonko