• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Utarukwa 2022, Ruto aonya Raila

Utarukwa 2022, Ruto aonya Raila

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto amemuonya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba ataona kivumbi iwapo anasubiri kuungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto alidai kwamba Bw Odinga alisambaratisha muungano wa NASA na kisha akatumia handisheki yake na Rais Kenyatta kuvunja chama cha Jubilee ili kishindwe kutimiza ajenda zake za maendeleo badala ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

“Niliwaambia hawa wangwana 2017 na wanarudia makosa yale yale waliyofanya. Hawana mipango, hawaelewi chochote na wakicheza hali itakuwa ilivyokuwa 2017,” alisema.

Akizungumza akiwa Kaunti ya Kilifi jana, Dkt Ruto alisema badala ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu, Bw Odinga na viongozi wengine wanaounga kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba wanasubiri kuidhinishwa na Rais Kenyatta kumrithi.

“Wale ndugu zetu na mimi nataka niwashauri kwa heshima. Niliwaeleza pale nyuma kwamba hawana mipango, shida ni kwamba bado wamekwama hapo. Mpaka saa hizi wanaitwa kikosi cha kubomoa kwa sababu walibomoa NASA na Jubilee,” alisema.

Alisema kwamba Bw Odinga na wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaounga BBI wako walipokuwa 2017.

KUTOKA KUSHOTO: Naibu Rais Dkt William Ruto, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika hafla ya wasilisho la kwanza la ripoti ya BBI katika jumba la Bomas hapo Novemba 27, 2019. PICHA/TONY KARUMBA / AFP

“Wako mahali walipokuwa siku ile. Jameni, saa hizi hamjielewi, hamjui kama mko upinzani au mko serikalini. Mambo yatakuwa yale yale halafu mtaenda kufanya uapisho feki,” alisema akirejelea tukio ambapo Bw Odinga alijiapisha rais wa wananchi Januari 30, 2018 kabla ya handisheki yake na Rais Kenyatta.

Dkt Ruto ambaye amepinga marekebisho ya katiba kupitia BBI alisema kwamba kwa sababu ya kukosa mpango, viongozi wa upinzani wanazunguka rais wakitaka awaunge mkono kuwa wagombea urais.

“Je mtu wa chama kingine, anawezaje kuidhinishwa na viongozi wa Jubilee. Wacheni utapeli, leteni sera zenu, sisi tumesema kwamba tunataka kuanzia chini kubadilisha uchumi, wacheni kuzunguka maofisi, mtakwama tena. Ukiona mtu ambaye yuko upinzani anasubiri kuidhinishwa na mtu aliye serikalini, hajielewi,” alisema.

Alisema kwamba Bw Odinga anataka kurejesha Kenya katika siasa za kikabila na kubadilisha katiba kubuni nafasi za uongozi kwa watu wachache.

Alisema kwamba wapinzani wake wanamkejeli kwa kuwa anaongoza juhudi za kuinua maisha ya watu wa mapato ya chini lakini akaonya kwamba hataacha kufanya hivyo.

“Wale ambao hawataki tuanze chini kwa watu wa mapato ya chini, waache madharau. Kazi ni kazi,” alisema.

Dkt Ruto alipuuza wanaodai kwamba anachochea vita vya matabaka kwa kusaidia watu wa mapato ya chini kujiinua kiuchumi.

Bw Odinga amekuwa akitaja kampeni ya Dkt Ruto ya kusaidia vijana kuanzisha biashara ndogo ndogo kama takataka.

Alidai kwamba ingawa Bw Odinga alivuruga ajenda za Jubilee, atatimiza zote akichaguliwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tulikuwa na manifesto ya Jubilee ambayo tuliorodhesha miradi na ajenda zetu lakini kwa sababu ya mambo haya, tukaambiwa eti kubadilisha katiba ndio nyadhifa zipatikane ndio dharura, tutatimiza yote tukitembea pamoja,” alisema.

Aliwarai viongozi wa pwani kuacha azima ya kubuni chama cha eneo lao na kuungana naye katika chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Dkt Ruto aliwahakikishia viongozi wa pwani kwamba hatawaruka wakimuunga kushinda urais.

“Shida ya matatizo ya siasa za Kenya ni utapeli, watu wakora wanaodanganya wengine wakati wa kampeni za uchaguzi na kisha kuwaruka wakiingia mamlakani,” alisema.

“Kwa hivyo, kama mnatafuta mtu muungwana anayetimiza ahadi na neno lake lina maana, njooni tutembee pamoja. Naambiwa mnapigia mtu kura kisha anawasahau,” alisema.

You can share this post!

Nina saini za wabunge 126 kumtimua Ruto – Savula

Hosea Kiplagat, mwandani wa zamani wa Mzee Moi, afariki