BBI yapanua ufa Bonde la Ufa

BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO

MGOGORO umeibuka miongoni mwa wanaounga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI) katika eneo lenye kura nyingi la Bonde la Ufa, kuhusu umilisi wa mchakato huo.

Haya yamejiri huku mchakato huo ukielekea katika mabunge ya kaunti.

Timu inayoongozwa na mwenyekiti wa ODM eneo la Elgeyo Marakwet, Micah Kigen, jana ilidai kuwa imetengwa katika mchakato wa kufanya maamuzi na timu ya msimamizi wa eneo hilo Alex Tolgos.

Walisema jambo hilo huenda likaathiri kiasi uidhinishaji wa ripoti hiyo.

“Tunataka timu zote zinazounga mkono BBI katika eneo hili kuhusishwa katika upigiaji debe ripoti hiyo kuhusu marekebisho ya katiba badala ya baadhi ya watu binafsi wanaotumia mchakato huo kwa maslahi yao wenyewe,” alisema.

Bw Kigen alitofautiana na timu ya Bw Tolgos kwa kile alichodai kama kuandaa warsha na mikutano katika hoteli za kifahari badala ya kuelimisha umma na kushawishi mabunge za kaunti katika ngome ya Naibu Rais William Ruto na kupitisha nakala kuhusu mswada huo wa kufanyia katiba marekebisho.

“Pana haja ya kutumia mikakati jumuishi kuhakikisha kwamba kaunti kutoka eneo hili haziachwi nyuma katika upitishaji wa mswada ambao ni muhimu kwa watu wetu,” alisema.

Haya yamejiri huku timu ya Gavana Tolgos ikijitahidi kupuuzilia mbali propaganda inayosambazwa na wapinzani wao eneo hilo.

Viongozi hao wawili wanawategemea Seneta wa Baringo Gideon Moi, Gavana Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) na Lee Kinyanjui (Nakuru), Maseneta: Samuel Poghisio (Pokot Magharibi) na Profesa Margaret Kamar (Uasin Gishu), Wabunge: Joshua Kutuny (Cherang’any), Alfred Keter (Nandi Hills), Vincent Tuwei (Mosop), William Kamket (Tiaty) na Swarup Mishra (Kesses), kuongoza shughuli ya upigiaji debe BBI katika ngome ya kisiasa ya Naibu Rais.

Hatua hiyo huenda ikawakasirisha vigogo wa Chama cha Jubilee katika eneo hilo.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?