Nina saini za wabunge 126 kumtimua Ruto – Savula

Na BENSON MATHEKA

MIPANGO ya kumuondoa ofisini Naibu Rais William Ruto inayoshinikizwa na chama cha Amani National Congress (ANC), inaendelea huku tofauti zake na Rais Uhuru Kenyatta zikiendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa mbunge wa Lugari anayeongoza juhudi hizo, Ayub Savula, tayari wabunge 126 wametia saini mswada wake wa kumuondoa Dkt Ruto ofisini kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza na gazeti moja la humu nchini Alhamisi, Bw Savula ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ANC alisema kwamba ana hakika atapata wabunge wengine 107 wa upinzani kutimiza idadi inayohitajika kumtimua Dkt Ruto ofisini.

“Wale ambao wanasema kwamba chama changu hakina idadi ya kutosha ya wabunge kupitisha mswada huu hawajui kwamba wabunge wa vyama vyote kutoka kote nchini wanauunga mkono,” Bw Savula anasema.

Miito ya kumuondoa ofisini Dkt Ruto kwa madai kwamba anamkaidi rais inaendelea kushika kasi tangu mazishi ya mama ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi katika kaunti ya Vihiga mwezi jana.

Kwenye mazishi hayo, katibu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu) Francis Atwoli, Bw Mudavadi na seneta wa Kakamega Cleophas Malala walimtaka Rais Kenyatta kumwadhibu naibu wake wakisema anahujumu ajenda za serikali na kumdharau hadharani.

Rais Kenyatta aliyehudhuria mazishi hayo aliwajibu kwa kusema kunyamaza kwake hakumaanishi hafahamu kinachoendelea. “Ukiona simba amenyeshewa, usidhani ni paka. Kila kitu na wakati wake,” Rais alisema.

Kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohammed alimtaka Dkt Ruto kujiuzlu kabla ya kumuondoa ofisini kupitia bunge.

Bw Junet anamlaumu Dkt Ruto kwa kuacha majukumu yake kama msaidizi wa rais na kuzunguka nchini kupigia debe azma yake ya urais 2022.

“Nataka kumwambia Naibu Rais ajiuzulu kabla sijatumia bunge kumuondoa ofisini. Ameacha ofisi yake, huwa namuona kila mara akihutubia umati kando ya barabara sehemu tofauti nchini,” alisema Bw Junet mbele ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga katika jumba la ufungamano alipokutana na viongozi wa wanawake wa vyama vya Jubilee na ODM Kaunti ya Nairobi.

Washirika wa Dkt Ruto wamepuuza mswada wa Bw Savula wakisema kwamba kumuondoa naibu rais ofisini si rahisi.

Hata hivyo, akizungumza akiwa Kakamega Alhamisi, Bw Savula alisema kwamba ana hakika atashawishi wabunge 233 wanaohitajika kuunga mswada wake kumuondoa Dkt Ruto ofisini.

Asema Dkt Ruto amekuwa akimhujumu Rais Kenyatta ingawa walichaguliwa pamoja.

“Rais anajaribu juu chini kutekeleza ajenda za serikali yake alivyoahidi Wakenya lakini anachofanya naibu wake ni kumhujumu kwa kumkaidi hadharani. Hivi sivyo serikali inavyofaa kuhudumu,” alisema.

Aliunga kauli ya Bw Junet kwamba Dkt Ruto anafaa kujiuzulu kabla ya kutimuliwa ofisini.

Juhudi za kumuondoa Dkt Ruto zinaonekana kuwa za kumzuia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza akiwa Kabarak alipohudhuria makumbusho wa mwaka wa kwanza tangu kifo cha aliyekuwa rais wa pili wa Kenya Daniel Moi, Rais Kenyatta alimlaumu Dkt Ruto kwa kukosa unyenyekevu.

Habari zinazohusiana na hii

Ruto amhepa Uhuru

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto