• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
DOUGLAS MUTUA: Polisi pia ni watu, watunzwe ndipo wapate ari kutulinda

DOUGLAS MUTUA: Polisi pia ni watu, watunzwe ndipo wapate ari kutulinda

Na DOUGLAS MUTUA

NIMEJIPATA nikitafakari sana kuhusu maisha ya polisi wa Kenya baada ya kushuhudia maombolezi ya kifo cha ofisa wa polisi aliyeuawa kwenye majengo ya bunge la Marekani.

Ofisa huyo, Bw Brian Sicknick, aliyeuawa na waandamanaji waliovamia majengo hayo yapata mwezi mmoja uliopita, aliagwa kwa taadhima kuu na Serikali ya Marekani juzi.

Mwili wake ulipelekwa kwenye majengo ya bunge kama unavyofanyiwa wa kiongozi wa kitaifa. Rais Joe Biden alifika humo kutoa heshima zake za mwisho.

Shughuli za mabunge yote mawili – seneti na wawakilishi – zilisitishwa ili kuonyesha heshima na shukrani za mwisho kwa ofisa huyo aliyefariki akiwalinda waheshimiwa.

Pamoja na heshima zote hizo, makachero wa Marekani bado hawajamkamata mshukiwa yeyote kuhusiana na kifo cha ofisa huyo, wala kuamua watamshtaki nani.

Hawana hakika ni nani aliyehusika moja kwa moja na hawataki kuwabambikizia watu makosa kiholela tu ili wamalize uchunguzi mapema inavyofanyika nchini Kenya.

Kumbuka Kenya mtindo wa kawaida ni kuwakamata watu wengi tu, kuwapeleka mahakamani haraka na kuomba waruhusiwe kuwazuilia wakiwatafutia makosa!

Baada ya kushuhudia heshima alizopewa Bw Sicknick, nilitwaza kwa kina kuhusu maisha ya polisi wa Kenya, dharau wanazopitia na ugumu wa maisha kwa jumla.

Hata maofisa wanaowalinda waheshimiwa huchukuliwa kama majibwa yanayomfuata mtu na kumnusanusa tu akiwa kwenye shughuli zake za siku.

Waheshimiwa wengi nchini Kenya huwachukia na kuwadharau maofisa hao kwani wanawachukulia kama majajusi waliotumwa na Serikali kuwachunguza.

Nikikumbuka maofisa wa polisi wa Kenya ambao wameuawa wakiwa kazini na jinsi walivyozikwa na kusahaulika haraka, najiuliza iwapo kweli tunawathamini.

Wakumbuke waliouawa katika shughuli za kukabiliana na magaidi kisha ujiulize iwapo serikali iliwapa heshima walizostahili.

Kumbuka maafisa karibu 50 waliouawa na majangili eneo la Kapedo miaka kadhaa iliyopita na wengine hivi majuzi tu na maisha yakaendelea kana kwamba uhai wao si kitu.

Mauaji kama hayo yangetokea mahali kama Marekani, hiyo ingekuwa dharura ya kitaifa na kila mtu duniani angejua nchi hiyo inaomboleza.

Rais, hata akiwa katika ziara ya nje, angekatiza shughuli za siku na kurejea nchini mwake ili kuongoza maombolezi.

Hayo hayawezi kufanyika Kenya! Anayeuawa kazini husubiri ile suluti ya kufyatuliwa mizinga 21 wakati wa mazishi na basi! Hiyo haitoshi wala haifai kitu kwa kuwa ni kufuata kaida ya kitamaduni tu.

Kuthamini

Ofisa mlengwa, sawa na hali ilivyokuwa wakati wa uhai wake, hathaminiki kabisa kwa kufyatuliwa mizinga. Huo huwa ndio mwisho wa uhusiano wa serikali na familia yake.

Familia nyingi za maofisa wanaofia kazini nchini Kenya huishia kutaabika kiasi cha watoto kutosoma kwa kuwa polisi hawana bima ya maisha.

Wangewekewa bima hiyo na serikali, ugumu wa maisha ambao huzipata familia zao wakifariki unaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Kuwa na hakikisho kwamba hata ukiaga dunia ukiwa katika shughuli za kikazi familia yako itakuwa na kifutia machozi cha kuendelea na maisha ni kitu cha kuridhisha.

Naelewa vizuri tu kwamba Wakenya wengi wanawadharau na kuwachukia polisi kutokana na ufisadi, dhuluma na maonevu tele. Ni kawaida kutowapenda watesi wako.

Lakini pia ni vyema kujiuliza iwapo hali yao ya kuchukiza hiyo huzidishwa na mazingira ya kikazi. Labda wamekata tamaa, wakaamua kutafuta mbinu za kusalia hai tu.

Mwenyewe ukijua kesho ukifa utazikwa na kusahaulika kama mbwa, hutazua ujanja wa kujitafutia nafuu ya maisha?

Sitetei waovu na maovu yao; ninalosema ni kwamba polisi pia ni binadamu. Wajibu wanaotekeleza wa kulinda usalama ni wa kimsingi mno. Wakigoma hata dakika 30 tu utaona maajabu ya ulimwengu.

Tutakuwa tumeanza kuelekea mahali pazuri tutakapoanza kushughulikia maslahi ya polisi na kuwatunza kama binadamu wenzetu.

[email protected]

You can share this post!

Meneja aliyeghushi vyeti atafune mamilioni abubujikwa na...

CHOCHEO: Hadaa ya mapenzi huja na kilio