• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
THIS LOVE: Wakenya wawapongeza Nameless na Wahu kwa utunzi wa kipekee kukaribisha Valentino Dei

THIS LOVE: Wakenya wawapongeza Nameless na Wahu kwa utunzi wa kipekee kukaribisha Valentino Dei

NA WANGU KANURI

Mwezi wa Februari hunasibishwa sana na wengi kama mwezi wa mapenzi. Mwezi huu ambao una siku ya Valentino, huwaangazia wachumba wanavyonogesha mapenzi.

Siku hiyo ya Valentino, wapenzi na wapendwa wao huvalia mavazi mekundu ishara ya mapenzi. Maua ya waridi hupokezwa wanawake hii ikiwa siku ya wanaume kuonyesha mapenzi yao kwa wachumba wao.

Hoteli nazo hujizatiti katika kuhakikisha siku hii imefana kwa wapendanao. Aisee, mapenzi ni kama mti, penye mbolea hujiotea.

Hali kadhalika, mwezi huu wa Februari katika ulingo wa uanamuziki ulikuwa wa aina yake huku mahabubu wawili Nameless na Wahu wakiutoa wimbo almaarufu This Love.

Wimbo huu ambao ulizinduliwa siku mbili zilizopita, ulionyesha mtazamo sawa lakini maandishi na mIrindimo ya kingoma tofauti kwa wimbo huu.

Ni kweli kuwa mapenzi ni kama waridi, kuna nyakati ambazo mapenzi ni matamu na nyakati zingine mapenzi yayo hayo hugeuka shubiri.

Uzuri wake huwa katika pandashuka hizo za mapenzi. Kwa mtazamo huu This Love ya Wahu inashukuru uchangamfu na urembo wa uhusiano wa kimapenzi huku kupitia kwake mtu huwa na busara, huku This Love ya Nameless ikionyesha uchungu na ugumu ulio katika uhusiano wa kimapenzi huku ukimfanya mtu kuwa na busara katika mapenzi na maisha kwa ujumla.

Utunzi huu wa kipekee, unaoangazia mada sawa lakini mitazamo tofauti umekuwa wa kwanza katika ulingo wa utunzi wa nyimbo.

Wimbo huu uliwafanya wawili hawa kuvuma sana kwenye mitandao ya kijamii, huku wasanii hao wakiwarai mashabiki wao kupigia debe wimbo wao.

Hali kadhalika, utunzi huu umewafaa sana wasikilizaji kwani umeonyesha mwisho wa mapenzi unapaswa kuwa, kupata busara katika uhusiano huo wa kimapenzi na maisha kwa ujumla.

Wakenya hali kadhalika, hawakukosa kuibua gumzo na kutoa maoni yao katika mitandao ya kijamii kuhusiana na utunzi huu:

“Kama hujausikiza wimbo mpya wa #Nameless, nenda Youtube na ufanye hivyo, ni wimbo mzuri sana,” akaandika @ongodo_.

“Ninapenda mashindano haya yenye kujengana kati ya #Nameless na #Wahu,” akasema @naisula_sula.

“Ni Februari na ni mwezi wenye kuonyesha mapenzi. #Nameless na #Wahu wameutoa wimbo mpya na unapeperushwa moja kwa moja huko Youtube,” akaandika @KUcoolkid.

“Ninapenda mtazamo ambao #Wahu na #Nameless waliketi chini na kufikiria kuwa ni vyema wao kufanya wimbo kuhusu mapenzi na vile wawili hawa wameonyesha wanavyohisi kuhusu mapnezi,” akanena @RonnyReagan10.

“This Love ya #Nameless na #Wahu ni mzuri. Ubunifu mzuri kwenye video,” akasema @SamNato.

Ninapenda hujawahi nisikitisha, wimbo mtamu sana siwezi ngoja kumtabarukia mume wangu,” akaandika Annita Wanjiku.

“Huu ni wimbo mzuri. Sio kelele ambayo tumezoea,” akasema Njambi Njoroge.

“Wacha sote tujieleze kupitia nguvu za mapenzi, Amani na muziki,” akasema Arab Ganda.

“Kosa tu lililo katika video hii ni kuwa lina mwisho,” akaandika Kenndollartv.

“Hii ndiyo hali halisi ya vile Valentino itakuwa. Wengine watakuwa na furaha kama Wahu na wengine watakuwa kama Nameless. #NamelessnaWahu hongera kwa kina Mathenges,” akaandika Monicah Mungai.

“Wimbo huu unazungumzia watu wote kibinafsi,” akasema Robert Iena.

“Kila wakati ambapo unasikia Nameless ana wimbo mpya, kwa hakika unajua maudhui yamekomaa. Mapenzi mengi kwa Nameless, Wahu na familia kwa ujumla. Nimekuwa shabiki kutoka enzi,” akaandika Sir. Major Alex.

You can share this post!

Raila asema Ruto aliarifiwa kuhusu handisheki na Rais

Chelsea wabomoa Spurs