Ruto awafokea waliopeleka bandari kavu Naivasha

Na MOHAMED AHMED

NAIBU Rais William Ruto, amedai mradi wa usafirishaji mizigo kupitia reli ya SGR ulitekwa na matapeli ndipo biashara za Pwani zikafilisika.

Akizungumza jana katika eneo-bunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, Dkt Ruto alisema serikali ya Jubilee iliunda mradi huo ili kuwanufaisha wakazi wa Pwani, lakini vingozi wachache wameamua kutumia ushawishi wao kujinufaisha kibinafsi kwa kupeleka biashara nyingi za SGR maeneo ya Naivasha na Nairobi.

Kulingana naye, mpango wa serikali ulikuwa kwamba SGR ijengwe sambamba na bandari kavu ya Dongo Kundu ili kulinda biashara na uchumi wa Pwani, lakini mradi wa Dongo Kundu ukacheleweshwa kukamilika.

“Sisi hatukujenga SGR ili tudhulumu watu wa Mombasa ama kuondoa biashara hapa na kuzipeleka Nairobi ama Naivasha. Tulijenga SGR kwa ajili ya kupanua biashara. Lakini kuna watu wachache na matapeli ambao wamechukua mradi huo na kuutumia kuharibu biashara za watu wa Mombasa,” akasema Dkt Ruto.

Alisema kwa sababu hiyo kuna haja ya mipango kurekebishwa ili mradi huo ambao ulifaa kunufaisha biashara za watu wa Mombasa utimize dhamira hiyo.

“Mahali palipokuwa na kazi 100, pawepo kazi 200 na hilo litafanyika wakati mradi ule mwingine wa bandari huru utakapokamilika na kuwezesha wakazi wa Mombasa kunufaika kiuchumi,” akasema Dkt Ruto.

Hata hivyo, matamshi ya Dkt Ruto kuhusiana na kutekwa na watu wachache yanaenda kinyume na yale ya mkuu wake Rais Uhuru Kenyatta ambaye wakati alipozuru Mombasa alikana madai hayo kuwa mradi wa SGR unawakandamiza watu wa Mombasa.

Wakati wa ufunguzi wa mradi wa daraja la kuelea mnamo Desemba mwaka jana, Rais Kenyatta aliwakemea wale wanaodai kuwa mradi wa SGR umekuja kuharibu biashara za Pwani.

Rais Kenyatta alisema kuwa viongozi wanaopinga mradi huo hawana hoja isipokuwa siasa tu.

Baadhi ya viongozi akiwemo mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar wamekuwa wakiwakashifu Rais Kenyatta na Gavana Hassan Joho kwa kuwahadaa watu wa Pwani na kutumia mradi wa SGR kujinufaisha.

Bw Joho amepinga madai hayo.

Aidha, jana wakati wa ziara yake ya Pwani, Dkt Ruto pia aliwaahidi wakazi wa Mombasa kuwa watanufaika na miradi ya vijana wakati atakapokuwa rais wa tano wa nchi hii.

Dkt Ruto alisema kuwa viongozi wanampinga kwa sababu yeye ameshikana na wananchi.

Alisema kuwa viongozi hao wengine wanasubiri kukaa kwenye meza na kuwaamulia Wakenya yule atakayewaongoza.

“Ninyi mtakubali kuchaguliwa viongozi ama mutafanya uamuzi wenu wenyewe? Mimi ninawaomba tushikane pamoja na tutembee pamoja,” akasema Dkt Ruto.

Habari zinazohusiana na hii

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto