• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Nitamwambia Uhuru akutimue, Atwoli amtishia Kagwe

Nitamwambia Uhuru akutimue, Atwoli amtishia Kagwe

RUSHDIE OUDIA Na SAMMY WAWERU

Katibu Mkuu wa Cotu Bw Francis Atwoli amemtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kufutilia mbali notisi aliyotoa inayoagiza wahudumu wa afya kukomesha mchango wao katika vyama vya kuwatetea.

Bw Atwoli ameonya kuwa Waziri asipoondoa notisi hiyo, Cotu ambayo ni muungano wa kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini itamchukulia hatua za kisheria.

Alisema endapo Bw Kagwe hatafutilia mbali notisi hiyo, Cotu haitakuwa na budi ila kuelekea mahamakani au kuagiza Rais Uhuru Kenyatta kumtimua.

Kwenye notisi hiyo iliyotolewa mnamo Desemba 22, 2020, na kutumwa kwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Prof. Margaret Kobia, Bw Kagwe ameeleza kwamba uamuzi huo uliafikiwa baada ya Wizara ya Afya na Baraza la Magavana (CoG) kufanya mkutano siku iliyotangulia.

Inadokeza, Waziri Kagwe anaeleza iliamuliwa kuanzia siku iliyotolewa (notisi) wizara yake na serikali za kaunti hazitakuwa zikitoa ada hizo, katika idara ya afya.

Bw Atwoli hata hivyo amesema notisi hiyo ni haramu kisheria na kwamba inakiuka matakwa ya sheria za kazi.

“Tunaelewa baadhi ya wizara zina mazoea kukiuka maagizo ya korti. Tukielekea kortini, Waziri wa Afya atakumbana na muungano wa kutetea wafanyakazi nchini. Pia tutashinikiza Rais amfute kazi,” akaonya.

Alisema Kenya ni mwanachama wa muungano wa kimataifa kutetea wafanyakazi, ambao umeruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama au miungano ya kutetea haki zao, kujumuika kueleza mahangaiko yao na pia kuandaa mkataba wa makubaliano.

Bw Atwoli alisema haiwezekani serikali ya Jubilee kutoa ilani kwa idara zote, ikiagiza zisitoe ada za miungano inayojumuisha ya wauguzi, madaktari, matabibu na maafisa wa kliniki, pamoja na miungano mingine na watumishi wa umma.

“Serikali haiwezi ikabatilisha sheria iliyopitishwa 1965 – mwajiri anapaswa kutoa mchango wa mfanyakazi kutoka kwa mshahara wake, na kuuelekeza kwa muungano wa kutetea haki zake,” akaeleza katibu huyo mkuu wa Cotu.

Alisema mchango unaotolewa na wanachama wa miungano huwa kwa hiari, na ni haki yao.

Kisa cha wahudumu wa afya kuhujumiwa na serikali wasijiunge na miungano ya kutetea haki zao si ya kwanza.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Kutetea Walimu Nchini (KNUT), Bw Wilson Sossion, amekuwa akilumbana na tume ya kuajiri walimu, TSC, akiilaumu kusitisha mchango wa wanachama wake mwezi wa Julai, Agosti na Desemba 2019, na miezi iliyofuata.

Mbunge huyo maalum ananyooshea TSC kidole cha lawama kwa kuhangaisha walimu wanachama wa KNUT, hatua anayohoji inaenda kinyume na kifungu cha 48 cha Sheria ya Leba.

Anasema hatua hiyo inalenga kulemaza nguvu za KNUT katika kutetea walimu nchini.

TSC hata hivyo imekana madai hayo.

You can share this post!

Muuguzi asimulia alivyolazimishwa kupashwa tohara akiwa na...

Wanawake Kenya hulipa maradufu kupata huduma za M-Pesa...