• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Utepetevu Kenya Power ulivyoiletea familia mahangaiko

Utepetevu Kenya Power ulivyoiletea familia mahangaiko

HELLEN SHIKANDA, FAUSTINE NGILA Na SAMMY WAWERU

Petronilla Muchele ni mama mwenye huzuni, huku uso wake ukieleza bayana anayopitia. Kitengo cha Afya, katika Meza ya Taifa Leo Dijitali kilipomtembelea nyumbani kwake, kilimpata kitandani akiwa na mwanawe wa kiume wa pekee, Isaac Matati.

Hali ya huzuni inatanda nyumba ya mkazi huyo wa eneo la Uthiru, kiungani mwa jiji la Nairobi, anaposimulia mwanawe huyo wa kiume alivyogongwa na waya yenye nguvu za umeme Alhamisi moja Okotoba mwaka uliopita.

Ni mkasa ambao umesababisha familia yake kupitia mahangaiko. “Niligundua siku iliyofuata mmoja wa wanafamilia aliponiarifu alikanyaga waya yenye nguvu za umeme, ambayo ilimuacha katika hali mbaya. Aliniambia amekimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” mama huyo wa watoto wanne anakumbuka, huku akibubujikwa na machozi.

Isaac, na ambaye kwa muda wa majuma saba asingeweza kujigeuza kitandani baada ya mkasa, ameruhusiwa kuondoka hospitalini, ila ana mahangaiko.

Ana matatizo ya kuketi chini, jambo ambalo linamlazimu kusalia kitandani siku nzima. Kijana huyo anatusimulia alivyokumbana na mkasa, akidokeza kwamba alikuwa akifuata njia katika barabara ya Chiromo ili avuke kuelekea eneo la Villa Rosa Kempsinki, Nairobi, kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha, alipokanyaga waya yenye nguvu za umeme.

“Sehemu ya mguu kati ya suruali ndefu na viatu ndiyo ilipatana na waya wa stima. Nilipata fahamu nikiwa hospitalini bila uwezo wa kuzungumza wala kujigeuza. Mama ndiye alijukumika kunitunza kipindi ambacho nililazwa hospitalini,” baraobaro huyo mwenye umri wa miaka 31 anaelezea.

Ni ajali ambayo ilisitisha kwa muda ndoto zake kuwekeza katika biashara ya nguo na uchukuzi.

Petronilla anasema hali ya Isaac inamtatiza kimawazo, akizongwa na maswali chungu nzima wakati mwanawe ataweza kutembea tena, huku akikashifu kampuni ya usambazaji nguvu za umeme nchini, Kenya Power, kwa utepetevu wake kuachilia waya hatari kusalia ardhini kiholela.

Petronilla aonyesha picha ya mwanawe baada ya kupigwa na stima Westlands. PICHA/ LUCY WANJIRU

“Hata baada ya kuripoti na kuwaarifu hawajachukua jukumu la kuja kuona kijana wangu. Fedha tulizokuwa tumeweka kama akiba zimeisha, tunahangaika,” mama huyo ambaye ana umri wa miaka 56 na mchuuzaji wa mboga soko la Uhtiru analia akikadiria mahangaiko wanayopitia kufuatia utepetevu wa Kenya Power.

Stakabadhi za matibabu zinaonyesha Petronilla ametumia zaidi ya Sh400, 000, huku bili jumla ambayo KNH inadai familia hiyo na ambayo kwa sasa haina mbele wala nyuma ikiwa Sh2 milioni.

Isaac hata kabla ya ajali hiyo asingemudu kulipa bima ya afya ya Sh500 kwa mwezi kwa sababu ya ukosefu wa ajira. Familia yake kwa sasa inategemea msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Mkasa huo ulibadilisha maisha ya kijana huyo, hali ya upweke ikiendelea kumkumba hasa akiwa peke yake. Miguu yake hadi kwenye mapaja, shingo na koo ingali na makovu ya majeraha, siku za kwanza baada ya ajali akishindwa kumeza chakula.

Ni huzuni, hasa ikizingatiwa kuwa ni vigumu kumtambua kwa sababu ya jinsi uso wake uliharibiwa na makali ya nguvu za umeme. Familia yake na marafiki pekee ndio wanaweza kumtambua. Ni hali anayosema imemrejesha nyuma kimaisha.

Machozi yalikuwa yanambubujika wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali katika kibanda chake cha mboga mtaani Uthiru,Nairobi. PICHA/ LUCY WANJIRU

Kwa mujibu wa ripoti ya matibabu ya KNH, inaonekana Isaac alipooza na ambapo anapitia nyakati ngumu kuenda haja kubwa na pia ndogo.

Mama yake anasema hana nguvu wala uwezo kuendelea kutafutia familia yake riziki na pia kumtunza mwanawe, ambaye sasa amesalia kitandani.

“Nimesawijika, ila lazima nijikaze na kujituma kwenye biashara yangu anga tusukume gurudumu la maisha,” anaelezea, akifichua kwamba biashara yake humuingizia faida ya Sh300 pekee kwa siku.

Maelfu ya kesi yamerundika kortini, Wakenya wakiishtaki Kenya Power kufuatia visa vya watu na mifugo kugongwa na nyaya zenye nguvu za umeme, na kusababisha maafa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw Bernard Ngugi alinukuliwa awali akisema shirika hilo la usambazaji wa nguvu za umeme nchini linaendeleza kampeni kufuatia ongezeko la visa vya umma kuhangaishwa na stima, ambapo umma unaelemishwa athari zinazotokana na matumizi mabaya ya stima.

“Tuna jukumu kuhakikisha tunalinda maisha ya watu na kutoa huduma katika mazingira salama,” akasema.

Hata hivyo, watu wanaendelea kuhangaishwa na utepetevu wa kampuni hiyo na uunganishaji wa nyaya isivyofaa, ambapo nyaya zenye hitilafu zikiongoza kwa visa vya watu wanaoangamizwa na nguvu za umeme kwa asilimia 24, nyaya zilizounganishwa kwa njia haramu asilimia 16, nyumba na majengo yaliyo karibu na vikingi na nyaya za stima asilimia 12 na wanaocheza na umeme kiholela asilimia 9, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa 2020.

Takwimu zinaonyesha visa sita vya ajali inayosababishwa na nguvu za umeme Kenya huripotiwa kila mwezi, zaidi ya asilimia 32 ya visa hivyo vikitajwa kushuhudiwa katika makazi ya watu kwa sababu nyaya hafifu na mbovu na zilizounganishwa kwa njia haramu.

Utafiti pia unaonyesha kaunti 10 nchini zinazoongoza kwa visa vya watu kuangamizwa na nguvu za umeme na wengine kuachwa na majeraha mabaya zinajumuisha Nakuru, Nairobi, Kericho, Uasin Gishu, Siaya, Busia, Nyamira, Meru, Kirinyaga na Kiambu.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, wawili hao, Petronilla na mwanawe, wanaendelea kuzongwa na msongo wa mawazo, ambao ni hatari.

Katika kibanda chake cha mboga, mama huyo hana motisha kamwe anapohudumia wateja. “Huwazia jambo moja pekee usiku na mchana, mvulana wangu. Huwa sipati hata lepe la usingizi usiku kucha,” anasema, akionekana kulemewa na majonzi.

Maisha ya Isaac Matati yamekwama kwani hana uwezo wa kubadilisha hali ilivyo kwa sasa. PICHA/ KANYIRI WAHITO

Isitoshe, mama huyo amepoteza hamu ya mambo mengi hasa kula na kunywa, akiendelea kujisaili “kwa nini mwanangu akumbane na mkasa huo ambao sasa umekuwa donga ndugu?”

Kwa Isaac, ambaye hana budi ila kuitikia, itamchukua muda wa miaka miwili ili kupata nafuu, anaendelea kupoteza matumaini. Maisha ya marafiki zake yanaendelea kama kawaida, huku yake yakiwa yamesitishwa.

“Maisha yangu yamekwama kwani sina uwezo kubadilisha hali ilivyo kwa sasa,” anasema barobaro huyo. Kulingana na mwanasaikolojia Lukoye Atwoli baadhi ya matukio huchangia mahangaiko ya mawazo kwa mwathiriwa.

“Mwathiriwa anapaswa kukuza tabia binafsi ya kukubali matukio, hulka muhimu kudhibiti mawazo,” anasema mtaalamu huyo. Anasema baadhi ya matukio yanaweza kubadilisha namna mtu anawaza kuhusu mazingira na kinachomzingira.

Kulingana na Jarida la Science Daily, matatizo ya kimawazo kama vile Kisaikolojia, Mania,Msongo wa mawazo, Msongo wa mawazo unaojiri baada ya tukio hatari, matatizo ya kuzungumza na kubadilisha tabia ya maisha, na Kichocho ni kati ya mahangaiko yanayosababishwa na athari za nguvu za umeme.

“Dalili huanza kushuhudiwa siku kadha au baada ya miaka baada ya tukio,” Jarida hilo linaeleza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, matatizo ya kiakili ni kati ya magonjwa ambayo yamepuuzwa katika sekta ya afya, ikikadiriwa kuwa watu wapatao bilioni moja duniani wanaishi na matatizo ya kiakili.

“Mataifa mengi hutumia wastani wa asilimia 2 ya mgao wa bajeti yake kuangazia masuala ya kiakili. Licha ya baadhi ya nchi kuonekana kuongeza mgao, hauzajidi asilimia 1,” anaeleza Dkt Ingrid Daniels, ambaye ni Rais wa Muungano wa Matatizo ya Kiakili Dunaini, akihimiza mataifa kuchukulia masuala ya kiakili kwa uzito kwa minajili ya siku za usoni.

You can share this post!

Wanawake Kenya hulipa maradufu kupata huduma za M-Pesa...

Tangatanga Pwani wakata tamaa ya kuunda chama, wataingia UDA