Ruto asisitiza atakuwa pasta akistaafu siasa

VALENTINE OBARA na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto, amesisitiza msimamo wake kwamba atajitosa katika uhubiri atakapostaafu siasa.

Akizungumza Jumapili katika kanisa la Anglikana la All Saints Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, Dkt Ruto alitumia muda wake mwingi kuhubiria waumini badala ya kupiga siasa ilivyo kawaida yake.

Baada ya mahubiri yake, aliwaambia waumini na viongozi wa kanisa hilo wamtarajie kuwa mhubiri katika miaka ya usoni.

“Sijahitimu kuwa mhubiri kwa sasa lakini pengine nikimalizana na haya mambo ya siasa, nina mpango wa kuwa mhubiri,” akasema.

Naibu Rais alikuwa mhubiri katika miaka yake ya ujana alipokuwa mwanafunzi wa sekondari na baadaye chuo kikuu.

Kwingineko, wabunge wanaoegemea upande wa Dkt Ruto wanatarajiwa kukutana leo nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi kujiandaa kwa ufunguzi wa bunge la kitaifa hapo Jumanne. Mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa BBI na Bajeti ya Kitaifa ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa.

Chaguzi ndogo za useneta wa Machakos na katika maeneobunge ya Matungu na Kabuchai pia zitajadiliwa.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Dkt Ruto kimedhamini wagombeaji katika chaguzi hizo.

Hata hivyo, wabunge wandani wa Dkt Ruto wamekana madai kuwa mkutano huo unalenga kupanga mikakati ya kuhujumu ajenda za serikali katika bunge la kitaifa na seneti, mabunge hayo yanaporejelea vikao.

“Ndiyo tutakuwa na mkutano wetu wa kawaida wa kundi la wabunge wanachama wa vuguvugu la ‘hasla’ katika makao ya Naibu Rais. Tunalenga kuchukua msimamo kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa yenye faida kwa walala-hoi; lakini hatunuii kupinga mambo ya serikali bungeni,” Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi akaambia Taifa Leo.

Naye Mbunge wa Soy Caleb Kositany alisema wanakutana kujadili hatima yao katika chama cha Jubilee na kuratibu muskabali wao wa kisiasa uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

“Mkutano wetu hautajadili BBI na kura ya maamuzi inavyodhaminiwa kwa sababu hayo na masuala yasiyo na umuhimu wowote kwa raia wa kawaida kama vile mama mboga na wana bodaboda. Tunakutana kuratibu namna ya kufanikisha mipango ya kufanikisha mahitaji yao tutakapoingia mamlakani 2022,” akaeleza Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee.

Lakini duru zimesema kuwa mkutano huo ambao utahudhuriwa na karibu wabunge na maseneta 150 utajadili mbinu za kuhujumu mchakato kwa BBI kwa kupinga mswada wa kura ya maamuzi na mgao wa fedha za kufadhili kura maamuzi.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

Watermelon mpya?

BBI: Ruto atapatapa

Mambo yaenda segemnege