• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
Papa Francis achagua mwanamke katika baraza kuu

Papa Francis achagua mwanamke katika baraza kuu

Na MASHIRIKA

PAPA Francis amevunja desturi za Kanisa Katoliki kwa kuteua mwanamke awe katibu wa baraza kuu la maaskofu.

Hii ni mara ya kwanza kwa mwanamke kushikilia wadhifa huo katika baraza hilo linaloamua masuala ya dini.

Nathalie Becquart ambaye ni Mfaransa ni mmoja wa makatibu wawili waliotangazwa Jumamosi.

Alikuwa mshauri wa baraza hilo tangu mwaka wa 2019.

Hatua hii ya Papa Francis imedhihirisha azma yake ya “kutaka wanawake zaidi wahusike katika shughuli za kufanya maamuzi ya kanisa”, hii ni kwa mujibu wa Kadinali Mario Grech ambaye ndiye katibu mkuu wa baraza kuu la maaskofu.

“Katika miaka iliyopita, idadi ya wanawake walioshiriki shughuli za baraza kama wataalamu na wasikilizaji ilikuwa ikiongezeka. Uteuzi wa Mtawa Nathalie Becquart na uwezo wake kupiga kura, umefungua mlango mpya,” akasema Mario.

Baraza hilo husimamiwa na maaskofu na makadinali ambao wana haki za kupiga kura, na huwa kuna wataalamu wasio na mamlaka ya kupiga kura kuhusu maamuzi yanayotoa mwongozo kwa Kanisa Katoliki ulimwenguni.

Mkutano ujao wa baraza hilo umepangiwa kufanyika mwaka wa 2022.

Mkutano maalumu uliofanywa Amazon mwaka wa 2019 ulihudhuriwa na wanawake 35 walioalikwa lakini hakuna yeyote kati yao aliyekuwa na mamlaka ya kupiga kura.

You can share this post!

Ruto asisitiza atakuwa pasta akistaafu siasa

Kane ashiba sifa za Mourinho baada ya kubeba Spurs dhidi ya...