• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Manchester City waponda Liverpool na kujiweka pazuri kutwaa taji la EPL msimu huu

Manchester City waponda Liverpool na kujiweka pazuri kutwaa taji la EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walipiga hatua kubwa katika kuweka wazi maazimio yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kupokeza mabingwa watetezi Liverpool kichapo cha 4-1 mnamo Jumapili usiku.

Mchuano huo ulishuhudia chipukizi Phil Foden akitamba zaidi uwanjani huku masihara ya kipa Alisson Becker yakichangia pakubwa masaibu ya Liverpool wanaotiwa makali na kocha Jurgen Klopp.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu 2003 kwa Man-City kusajili ushindi dhidi ya Liverpool katika EPL ugani Anfield na ilikuwa pia mara ya kwanza kwa mkufunzi Pep Guardiola kuangusha Liverpool ugenini.

Kiungo raia wa Ujerumani, Ilkay Gundogan aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao katika dakika ya 49 baada ya kupoteza penalti katika kipindi cha kwanza.

Penalti iliyopotezwa na Gundogan ilitokana na tukio la fowadi Raheem Sterling kukabiliwa visivyo na kiungo mkabaji Fabinho ambaye kwa sasa hutegemewa na Liverpool kwenye safu ya ulinzi kutokana na wingi wa visa vya majeraha kambini mwa kocha Klopp.

Mohamed Salah aliwasawazishia Liverpool kupitia penalti katika dakika ya 63 baada ya kukabiliwa visivyo na beki Ruben Dias.

Hata hivyo, Alisson aliadhibiwa vikali kutokana na masihara yake yalimshuhudia akitatizwa pakubwa na Foden aliyechangia bao la pili lilifumwa wavuni na Gundogan katika dakika ya 73 kabla ya Sterling kufunga la tatu dakika tatu baadaye. Foden ndiye aliyezamisha kabisa chombo cha Liverpool katika dakika ya 83.

Ushindi kwa Man-City uliwadumisha kileleni mwa jedwali kwa alama 50, tano zaidi kuliko nambari mbili Manchester United. Ni pengo la alama 10 ambalo kwa sasa linawatenganisha Man-City na Liverpool wanaoshikilia nafasi ya nne.

Nafuu zaidi kwa Man-City ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Man-United, Liverpool, Leicester City na Chelsea ambao pia ni wagombezi halisi wa taji la EPL muhula huu.

Man-City walishuka dimbani wakilenga kulipiza kisasi dhidi ya Liverpool ambao waligeuka kuwa mwiba mchungu kwao tangu wajitwalie huduma za kocha Klopp mnamo Oktoba 2015.

Japo Liverpool walikosa huduma za mabeki matata, Man-City pia walikuwa bila maarifa ya kiungo Kevin de Bruyne na fowadi Sergio Aguero.

Mbali na masihara ya Alisson, mabeki Trent Alexandre-Arnold na Andy Robertson walizidiwa maarifa na Sterling na Foden kila Man-City walipoamua kufanya mashambulizi.

Liverpool wamesajili matokeo duni uwanjani Anfield tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na ndicho kikosi cha kwanza baada ya Chelsea mnamo Machi 1956 kuwahi kupoteza mechi tatu mfululizo za nyumbani wakiwa mabingwa watetezi wa EPL.

Kufikia wakati kama huu katika kampeni za EPL mnamo 2019-20, Liverpool walikuwa wakijivunia alama 67 kutokana na mechi 23. Ina maana kwamba miamba hao wamepungukiwa na pointi 27 kwenye rekodi waliyojivunia kufikia hatua kama hii kwenye kivumbi cha EPL katika muhula uliopita.

Liverpool watakuwa wageni wa Leicester City katika mchuano wao ujao wa EPL ugani King Power huku Man-City wakiwaendea Swansea City kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA mnamo Februari 10 kabla ya kuwaalika Tottenham Hotspur kwenye EPL wikendi hii uwanjani Etihad.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kane ashiba sifa za Mourinho baada ya kubeba Spurs dhidi ya...

Bunge la Kaunti ya Kiambu kujadili ripoti ya BBI