ONYANGO: Uhuru atufafanulie zaidi kuhusu wizi wa mabilioni

Na LEONARD ONYANGO

TANGU Rais Uhuru Kenyatta alipofichua mwezi uliopita, kuwa Sh2 bilioni huibwa kila siku kutoka serikalini, suala hilo limeendelea kusalia kitendawili.

Alipokuwa akizungumza katika mahojiano na vituo vya redio vinavyotumia lugha ya Kikuyu, Rais Kenyatta alisema kuwa fedha zitakazotumika katika kura ya maamuzi ya kutaka kurekebisha Katiba kulingana na mapendekezo ya mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), si kitu ikilinganishwa na Sh2 bilioni ambazo huibwa kila siku serikalini.

Kulingana na Rais Kenyatta, kura ya maamuzi itagharimu takribani Sh2 bilioni na wala si Sh14 bilioni kama ilivyokadiriwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kauli ya Rais Kenyatta kuhusu wizi wa Sh2 bilioni kwa siku iliwaacha Wakenya vinywa wazi huku wakishangaa kwa nini kiongozi wa nchi hajawachukulia hatua watu hao wanaoiba fedha za umma.

Ikiwa kauli hiyo ya Rais Kenyatta ndiyo hali halisi nchini, basi, Kenya imepoteza mwelekeo.

Fedha zinazoibwa ni nyingi zaidi kuliko Sh360 bilioni ambazo hutolewa kwa serikali za kaunti kila mwaka.

Hiyo inamaanisha kuwa kiasi kikubwa cha Sh6 trilioni ambazo serikali ya Jubilee imekopa tangu kuingia mamlakani 2013, zimeishia katika mifuko ya watu wachache.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, kiasi kikubwa cha fedha zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo pia haziwafaidi Wakenya.

Mathalani, ripoti iliyotolewa Novemba mwaka jana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, ilionyesha kuwa miradi ya zaidi ya Sh360 bilioni iliyoanzishwa na serikali ya kitaifa na kaunti imekwama au kutelekezwa kote nchini.

Kulingana na Bi Gathungu, miradi hiyo imetelekezwa kutokana na ukosefu wa hela au mivutano ya kisiasa.

Kauli hiyo ya Rais Kenyatta kuhusu wizi wa fedha imewakanganya Wakenya na sasa inatumiwa na wanasiasa kujipigia debe.

Kwa mfano, kambi ya Naibu wa Rais William Ruto imekuwa ikieleza Wakenya kuwa Sh2 bilioni zinazopotea kwa siku zilianza kuibwa baada ya mwafaka wa kisiasa baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, maarufu handisheki, mnamo 2018.

Kila siku ifikapo jioni, wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto wamekuwa wakikumbusha Wakenya kupitia mitandao ya kijamii kuwa: “kumbukeni tunapoenda kulala Sh2 bilioni zimeibwa”.

Kulingana na wanasiasa wa Tangatanga, fedha hizo zimekuwa zikiibwa na wanaounga mkono BBI.

Kwa upande mwingine, wanasiasa wanaounga mkono BBI wamekuwa wakisema kuwa fedha hizo zinazodaiwa kuibwa zinaporwa na wanasiasa wa Tangatanga.

Ikiwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeshindwa kuwanasa wanaoiba Sh2 bilioni kwa siku, serikali iwataje wezi hao.

Walipa ushuru wana haki ya kujua jinsi fedha zao zinatumiwa.

Serikali haina budi kujitokeza na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na kauli hiyo ya rais kuhusiana na wizi wa Sh2 bilioni kwa siku.

Habari zinazohusiana na hii