WARUI: Serikali ijitahidi kukomesha uhuni unaoendelea shuleni

Na WANTO WARUI

VISA vinavyoendelea hivi sasa vya utovu wa nidhamu shuleni havifai kutazamwa kwa macho tu. Kuendelea kukemea na kulaani vitendo hivi vya kihuni bila kuchukua hatua hakusaidii chochote.

Wanafunzi wanapoamua kuchoma mabweni yaliyowachukua wazazi na serikali mamilioni ya pesa kuyajenga kisha waepuke adhabu ya vitendo vyao, basi serikali itakuwa imefeli katika wajibu wake wa kulinda maisha na mali.

Kujaribu kutoa sababu kuwa huenda wanafunzi wanatumia mihadarati shuleni bila kuchunguza kiini chake hasa na kutafuta suluhisho ni sawa na kujaribu kuhalalisha mhalifu aliyefanya uhalifu na kumwachilia huru.

Tunapofikia kiwango cha kuwa walimu wanatekeleza majukumu yao kwa uoga na hofu ya maisha yao, sababu yoyote haiwezi kutolewa kuwapa amani na utulivu. Ni sharti walimu, kama wafanyakazi wengine wa serikali, walindwe na wapewe mazingira salama ya kufanyia kazi.

Sheria inayolinda haki za watoto aidha inahitaji kutafsiriwa vyema. Pengo la utafsiri wa sheria hiyo ndilo linalosababisha maafa haya. Kwamba mwanafunzi amelindwa na sheria ili asiadhibiwe kwa kiboko si kumaanisha kuwa mwanafuzi aachiliwe afanye atakavyo.

Sheria ipo ambayo inaelezea waziwazi ni hatua gani ambazo zinahitaji kuchukuliwa ikiwa mtoto wa chini ya miaka 18 amevunja sheria.

Isitoshe, kuna jela kadhaa za watoto nchini na shule za kurekebishia tabia. Wanafunzi ambao wanatekeleza maovu shuleni wanafaa kukamatwa na kupelekwa katika sehemu hizo. Wakati ambapo wanafunzi wanawaona wenzao wakichoma shule na hakuna adhabu yoyote inayotolewa, basi nao wanavionea fahari vitendo vile na kuvitenda ili nao wapate ‘sifa’.

Matumizi ya dawa za kulevya kwa wanafunzi huenda yamechangia sana. Kipindi kirefu ambapo wanafunzi walikaa nyumbani kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19 kuliwapa wanafunzi wengi fursa ya kujiingiza katika maovu. Wengi wa watoto wa kiume hasa wale wa shule za sekondari walitoka nyumbani punde tu wazazi walipoenda kazini.

Kuna wale walioweza kuajiriwa kazi za vibarua, hivyo basi kupata pesa ambazo hazikuwekewa bajeti yoyote. Pesa hizi ndizo zilizotumika kununulia mihadarati kama vile pombe na bangi. Iwapo wanafunzi kama hawa ndio ambao wamerudi shuleni na kuchanganyika na wengine bila shaka ni lazima watatekeleza uhuni.

Umefika wakati sasa ambapo Wizara ya Elimu na ile ya Usalama wa ndani zinahitaji kuja pamoja na kukabiliana na uhuni huu bila kukawia. Endapo hatua kali zitachukuliwa kwa haraka, wanafunzi watalainika na kukomesha maovu haya.

Hali ilivyo sasa ni kama Wizara ya Elimu imetiwa shemere na wanafunzi na inajitazamia tu bila uwezo wa kufanya chochote. Kulaani vitendo hivi vya uhuni bila kuchukulia wahalifu hatua za kisheria hakuna maana kabisa!

Habari zinazohusiana na hii