• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 7:55 AM
Kiplagat, kigogo wa enzi ya Moi aliyedaiwa kope

Kiplagat, kigogo wa enzi ya Moi aliyedaiwa kope

Na BRIAN WASUNA

MWAKA wa 2003 ulikuwa mwamko mpya kwa wandani wengi wa aliyekuwa rais, marehemu Daniel arap Moi, na Hosea Mundui Kiplagat alikuwa mmoja wa waliopata pigo wakati Emilio Mwai Kibaki alipoapishwa kuwa rais mpya.

Katika utawala wa Moi, hakuna yeyote ambaye angethubutu kujaribu kuwawinda wandani wake kama vile Kiplagat, ambaye alifariki wikendi, kwani walihofia adhabu kali kutoka kwa serikali.

Marehemu ambaye alikuwa mwana wa Isaac na Zipporah Salgong, alifariki Februari 6, 2021, alipokuwa anakimbizwa hospitalini na familia yake baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kwa Bw Kiplagat, kipindi cha baada ya utawala wa Moi kilimrusha katika masaibu ya kuandamwa na wapigaji mnada na watu wengine waliodai ni wamiliki halisi wa ardhi alizokuwa nazo.

Kabla kufariki kwake, alikuwa na kesi nyingi mahakamani za kujaribu kuokoa mali yake ikiwemo kipande cha ardhi Nakuru alichozozania na mwekezaji wa sekta ya utalii, Bw John Allan Okemwa.

Kesi nyingine ilihusu mzozo kati yake na jirani mtaani Karen ambaye alidaiwa kuchimba kisima karibu na boma la Bw Kiplagat.

Kando na kuwa mwandani mkubwa na mshauri wa Mzee Moi, marehemu alikuwa ni jamaa ya kiongozi huyo aliyetawala kwa miaka 24. Mama zao walikuwa binamu.

Kwa marafiki wake, alifahamika vyema kama HK. Ni kwa sababu hii ambapo hata mahakamani kuna majaji waliokuwa wakimtambua kama HK hata kama jina lake kamili liliandikwa katika stakabadhi za kesi.

Shirika la kwanza lililomwandama marehemu Kiplagat kikamilifu ni Shirika la Kitaifa la Biashara nchini (KNTC), katika mwaka wa 2005.

Shirika hilo la kiserikali lilijaribu kupiga mnada gari lake aina ya Mercedes Benz na lingine la Mitsubishi Pajero. Alikuwa anamiliki magari hayo kupitia kwa kampuni yake ya Integrated Wood Complex.

Magari hayo yalikuwa yamenunuliwa kupitia kwa mkopo wa Benki ya Cooperative na yalikuwa bado yamesajiliwa kwa jina la benki hiyo.

Benki ilipinga mipango ya kuyapiga mnada, na kusema hasara ingekuwa kwa benki kama KNTC ingeruhusiwa kuyauza.

Mwaka huo huo, Bw Kiplagat alimshtaki mwekezaji John Allan Okemwa kwa madai ya kuingia katika ardhi yake bila ruhusa Nakuru.

Kesi hiyo ilichukua muda mrefu zaidi miongoni mwa nyingine, kwani ilikamilika katika Mahakama ya Rufaa mwaka wa 2018 ambapo Bw Okemwa alipewa umiliki wa ardhi hiyo.

Mwezi uliopita, Jaji wa Mahakama Kuu, Bw David Majanja, aliruhusu Bank of India kupiga mnada nyumba ya kifahari ya marehemu Kiplagat iliyo mtaani Karen, Nairobi ambayo inagharimu zaidi ya Sh455 milioni.

Benki hiyo ilikubaliwa pia kupiga mnada mali zake nyingine ambazo alimiliki mjini Eldoret, ingawa haikufichuliwa ni za thamani gani.

Marehemu alikuwa na deni la Sh271.4 milioni kwa Bank of India ambazo zilikuwa zimechukuliwa kupitia kampuni zake mbili. Kampuni hizo ni Eldoret Concrete Poles Limited (Sh86.11 milioni) na Timber Treatment International Limited (Sh185.3 milioni).

Katika kesi hiyo, ilifichuka kulikuwa na uwezekano mkubwa alikuwa amefilisika kwani mara kwa mara alikosa kutimiza maombi ya benki kulipa madeni yake walivyokuwa wamekubaliana.

You can share this post!

Mkenya Abud Omar azidi kutesa ligini Ugiriki

Pingamizi kwa Kidero akitaka kuwika kijijini