• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Varane asaidia Real Madrid kuzamisha Huesca ligini na kupunguzia Zidane presha ya kupigwa kalamu

Varane asaidia Real Madrid kuzamisha Huesca ligini na kupunguzia Zidane presha ya kupigwa kalamu

Na MASHIRIKA

BEKI Raphael Varane alifunga mabao mawili na kusaidia Real Madrid kutoka nyuma na kuchabanga Huesca 2-1 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ni matokeo ambayo yalimpunguzia kocha Zinedine Zidane presha ya kufutwa kazi na waajiri wake Real ambao kwa sasa wanajivunia alama 43, saba nyuma ya viongozi Atletico Madrid ambao wana mechi mbili zaidi za kutandaza.

Real ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga, wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama sawa na nambari mbili Barcelona huku pengo la pointi moja pekee likitamalaki kati yao na Sevilla wanaofunga mduara wa nne-bora.

Javi Galan aliwaweka Huesca uongozini katika dakika ya 48 kabla ya Varane kusawazisha katika dakika ya 54 kisha kupachika wavuni bao la pili la Real dakika sita kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Chini ya Zidane, Real walishuka dimbani wakiwa na rekodi duni ya kushinda mechi moja pekee kati ya tano za awali – matokeo ambayo yalimweka kocha huyo raia wa Ufaransa kwenye hatari ya kupigwa kalamu na waajiri wake.

Kwa upande wao, Huesca ambao kwa sasa wanavuta mkia kwa alama 16 kutokana na mechi 22 zilizopita, waliingia ugani wakiwa wameshinda michuano miwili pekee kati ya 21 ya awali. Bao ambalo Huesca walifungiwa na Galan lilichangiwa na Shinji Okozaki.

Nusura Rafa Mir anayechezea Huesca kwa mkopo kutoka Wolves afungie kikosi chake bao la pili katika dakika ya 52 ila akapaisha kombora lake juu ya mlingoti wa goli la Real ambao ni mabingwa watetezi wa taji la La Liga.

Bao la kusawazisha lililofungwa na Real lilichangiwa na frikiki ya Karim Benzema aliyeshirikiana vilivyo na Varane pamoja na Casemiro aliyemtatiza pakubwa kipa Alvaro Fernandez katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

TAFSIRI NA CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Raila aaibisha Rasanga na Obado kwa kuchelewa mkutanoni

Karua ashangaa jinsi BBI itakavyosaidia kaunti kupata mgao...