• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Karua ashangaa jinsi BBI itakavyosaidia kaunti kupata mgao zaidi wa fedha wakati ambapo taifa linadaiwa matrilioni ya pesa

Karua ashangaa jinsi BBI itakavyosaidia kaunti kupata mgao zaidi wa fedha wakati ambapo taifa linadaiwa matrilioni ya pesa

Na SAMMY WAWERU

AHADI serikali za kaunti zitapata mgao wa asilimia 35 ya makadirio ya bajeti kila mwaka ni hewa tu, kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua amesema.

Bi Karua amesema serikali za kaunti zinahadaiwa kuunga mkono na kupitisha mswada wa BBI, kwa msingi kuwa zitapata nyongeza ya fedha, jambo ambalo kulingana naye vigumu.

Waziri huyo wa zamani wa Sheria alisema ni muhimu walioingizwa kwenye mtego huo wa hadaa kufahamu kwamba serikali haina fedha.

Alisema matrilioni ya fedha ambayo Kenya inadaiwa baada ya serikali ya Jubilee kujiwekelea mzigo wa mikopo, ni ishara kuwa serikali haina pesa.

“Tunaelewa serikali imelemewa kulipa mikopo, ahadi ya mgao wa fedha asilimia 35 kwa kaunti itatoka wapi?” akataka kujua.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wamekuwa wakiendesha kampeni kupigia upatu BBI, na kulingana na Karua mpango huo wa maridhiano na unaopendekeza Katiba kukarabatiwa unalenga kunufaisha viongozi wenye tama za ubinafsi.

“Wanaounga mswada huo wanataka kukama Wakenya,” Bi Karua akaonya.

Rais Kenyatta amekuwa akidai BBI ikipitishwa eneo la Mlima Kenya litanufaika zaidi, kutokana na ongezeko la maeneobunge.

Hata hivyo, Karua amesema mahangaiko wanayopitia wenyeji wa eneo la Mlima Kenya ni yaleyale wanayopitia wananchi wa maeneo mengine.

“Mimi nimetoka eneo la Kati, ukweli ni kwamba matatizo ya watu wa Mlima Kenya si tofauti na ya maeneo mengine ya nchi,” akasema mgombea huyo wa ugavana Kirinyaga 2017.

Akirai Wakenya kutopitisha BBI, amewataka kuungana naye kuhamasisha mchakato wa hiari wa ‘Linda Katiba’ aliozindua.

“Wakenya watumie tovuti ya mchakato huo kuwasilisha jumbe zozote za hadaa kujaribu kuidhinisha BBI. Katiba inataka kuhujumiwa,” alisema, akidai serikali inatumia vibaya machifu na madiwani kulazimisha mswada huo alioutaja kuwa ‘haramu’ kuidhinishwa.

Alisema tovuti ya Linda Katiba imepokea malalamishi mradi wa Kazi kwa Vijana, waliopata nafasi ya ajira hiyo baadhi walishurutishwa kutia saini ili kuruhusu tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuidhinisha BBI.

“Kuna hadaa nyingi zilizopo kwenye mswada huo unaopendekeza nyongeza ya nafasi za viongozi. Hatujui iwapo baadaye pendekezo litakalofuata litakuwa la Rais aongeze muda wake kuwa mamlakani,” Bi Karua akatahadharisha.

You can share this post!

Varane asaidia Real Madrid kuzamisha Huesca ligini na...

Wanajeshi wa Ulinzi Stars wakabwa na Stima, Mathare ikipata...