TAHARIRI: Vikao vya bunge viwafae Wakenya

KITENGO CHA UHARIRI

BUNGE la kitaifa linatarajiwa kurudia vikao vyake leo baada ya likizo. Inavyoonekana, wabunge wanajiandaa kwa makabiliano makali ya kisiasa watakaporejelea vikao vyao.

Haitakuwa haki kwa mwananchi ikiwa cheche za siasa ambazo tumekuwa tukiona huku nje wakati huu wote zitaingizwa hadi ndani ya bunge.

Katika miezi iliyopita, shughuli za bungeni zilitatizika kwa kiwango fulani kwa sababu ya mivutano ya kisiasa.

Wabunge wanafaa kuelewa kuwa walichaguliwa kufanya maamuzi ambayo yanastahili kuboresha maisha ya kila mwananchi na taifa kwa jumla. Wakati malumbano ya vyama vya kisiasa yanapopenya hadi ndani ya bunge, yataathiri pakubwa maamuzi yanayofanywa.

Hii ni kutokana na kuwa maamuzi mengi hayatafanywa kwa msingi wa kujali maslahi ya umma bali kwa kutaka kuwafurahisha vigogo wa kisiasa. Wakati huu joto la kisiasa limezidi kwa sababu ya mswada wa marekebisho ya katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) na pia kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa 2022 unaendelea kukaribia.

Kampeni kuhusu masuala haya mawili zimezidi katika kila pembe ya nchi, na bila shaka, si siri kwamba wabunge wanapanga kuyapenyeza hadi ndani ya bunge kuanzia kesho watakapokutana.

Tumebakisha muda mfupi sana kabla uchaguzi ujao uandaliwe. Badala ya kutumia muda uliobaki kwa mizozo isiyo na msingi, ni heri wabunge wajikakamue kutekeleza ahadi walizotolea wananchi walipokuwa wakitafuta kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kuna wengi wao walisahau kabisa majukumu yao wakiwa na lengo la kufurahisha wakuu wao wa kisiasa pekee.

Wananchi wengi wanatatizika kwa sababu mbalimbali ikiwemo uchumi uliozorota hasa baada ya janga la corona kuingia nchini tangu Machi mwaka uliopita.

Haya ni mambo ambayo yangehitaji viongozi kujikakamua zaidi kuboresha maisha ya umma badala ya kujitosa kwa kampeni za mapema na mizozo inayogawanya nchi.

Ni matumaini yetu kwamba kipindi hiki kifupi kilichobaki kabla bunge la sasa livunjwe na wabunge kurudi uchaguzini, litatumiwa vyema kwa manufaa ya wananchi. Raia pia wawe katika mstari wa mbele kusisitiza kutolewa huduma bora na viongozi wao.

Habari zinazohusiana na hii