WANGARI: Mikakati jumuishi inahitajika kukomesha vurugu shuleni

Na MARY WANGARI

KATIKA siku za hivi majuzi, kumekuwa na misururu ya visa vya utovu wa nidhamu shuleni ambapo mabweni yameteketezwa na watu kujeruhiwa.

Visa hivyo vimekithiri mno kiasi cha kugeuza mazingira ya shule yaliyokuwa salama zaidi kwa wanafunzi baada ya nyumbani, kuwa eneo hatari mno ambapo chochote chaweza kutokea.

Ingawa hii si mara ya kwanza au jambo jipya kwa visa vya utundu kushuhudiwa katika taasisi za elimu, suala hili limeibua mjadala mkali na kusababisha wadau husika kusaili upya mikakati ya kudumisha nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Walimu na wahudumu wa shule pia hawajanusurika katika visa vya hivi punde huku baadhi yao wakigeuka wahasiriwa baada ya kushambuliwa na wanafunzi.

Hali kwamba wanafunzi sasa wamegeukia kubeba silaha shuleni wakiwa na nia ya kuwadhuru watoto wenzao au walimu, badala ya kutilia maanani masomo yao, ni ya kutisha mno.

Ni bayana kuwa kuna tatizo kijamii ambalo linapaswa kutatuliwa kwa dharura ili kurejesha utulivu shuleni.

Bila shaka, likizo ndefu ambapo watoto walilazimika kukaa nyumbani kutokana na janga la Covid-19 imechangia pakubwa.

Ni vigumu kukisia mshtuko, msongo kimawazo, athari kihisia na kisaikolojia zilizowakumba watoto baada ya kugundua kwamba nyumbani si paradiso salama jinsi walivyolelewa kuamini tangu walipozaliwa.

Baadhi yao walilazimika kutazama wasijue la kufanya wazazi wao wakipigana na hata kutengana, huku wengine wakinajisiwa, kujeruhiwa na kutendewa unyama wa kila aina na watu waliowaamini.

Katika juhudi za kutoroka uhalisia, baadhi ya watoto walianza kutumia mihadarati, kushiriki ngono kiholela na sarakasi nyinginezo mradi tu waweze kuendelea kuishi.

Si ajabu kwamba hatua ya kufungua shule nchini ilikuwa afueni kuu kwa wanafunzi lakini sasa walimu na wahudumu ndio wanaokumbana na makali ya watoto waliotatizika pakubwa.

Hisia mbalimbali zimeibuka kuhusu namna ya kurejesha nidhamu shuleni huku baadhi ya watu wakipendekeza kurejelewa kwa adhabu ya kiboko inayoaminika kukubalika hata katika vitabu vya kidini.

Sheria ya Watoto (2001) imepiga marufuku adhabu ya kiboko shuleni ikiwemo aina yoyote ya dhuluma na ukatili kwa watoto.

Isitoshe, Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyotia sahihi Mkataba kuhusu Haki za Watoto (1990) unaokataza adhabu ya kikatili.

Umuhimu wa kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi hauwezi ukapuuzwa pamoja na juhudi za kuwaelewa zaidi na kupata suluhisho la kudumu.

Juhudi za pamoja kutoka kwa wadau husika zinahitajika ili kurejesha hadhi ya taasisi za elimu kama mazingira salama kwa watoto kukua na kupata maarifa.

Habari zinazohusiana na hii