ODONGO: Wanasiasa wamakinike katika mchakato wa BBI

Na CECIL ODONGO

KASI ambayo Kaunti ya Siaya ilipitisha nayo ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) inaonyesha kuwa wanasiasa hawana haja na kusoma ripoti hiyo bali nia yao ni kuwaridhisha vigogo wa kisiasa hapa nchini.

Vivyo hivyo, kaunti ambazo zitaangusha ripoti hiyo zitafanya hivyo kwa sababu za utiifu kwa Naibu Rais Dkt William Ruto na wandani wake wa kisiasa ambao wamekuwa wakiipinga na kutaka msimamo wa pamoja uafikiwe kabla ya kura ya maamuzi.

Mnamo January 27, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilituma mswada wa BBI kwa kaunti zote 47 baada ya kuthibitisha saini milioni 1.1 zilizokusanywa kote nchini kuunga ripoti hiyo.

Hata hivyo, siku nane baadaye Kaunti ya Siaya ambayo ni nyumbani kwa kinara wa ODM Raila Odinga ilipitisha mswada huo upesi. Kisheria kaunti zina siku 90 kujadili na kupitisha ripoti hiyo lakini Siaya ilifanya hivyo kwa siku nane tu.

Kati ya maswali mazito ni je, wananchi walihusishwa vilivyo kuyafahamu yaliyomo kwenye BBI au madiwani wa Siaya walitaka kudhihirishia ulimwengu kwamba kwa kuwa Bw Odinga anatoka eneo hilo basi gatuzi hilo ndilo lilifaa kuwa la kwanza kupitisha ripoti hiyo?

Huu upepo wa kisiasa ndio ulitumika wakati wa kupitisha rasimu ya katiba ya 2010 ambapo wafuasi wa Bw Odinga hasa katika eneo la Nyanza walinukuliwa wakisema kuwa hawataisoma kwa sababu Bw Odinga alikuwa ashawasomea.

Si ajabu kwamba katiba hiyo ambayo imekuwa kwa miaka 10 pekee sasa inadaiwa ina kasoro ambazo zinafaa kusuluhishwa kupitia kwa ripoti ya BBI.

Isitoshe, si siri kwamba wengi wa madiwani wa Siaya ambao walipitisha mswada huo haraka haraka walifanya hivyo kwa sababu wanayaelewa masuala yaliyomo ndani.

Wengi wao walifanya hivyo ili kumridhisha Bw Odinga na kumdhihirishia kuwa wanaunga mkono BBI huku kaunti za Homa Bay, Kisumu na Migori nazo zinatarajiwa kuupitisha wiki hii.

Iwapo Gavana wa Siaya Cornel Rasanga, wabunge na viongozi wengine wangekuwa na kasi ya kutekeleza au kutimiza ahadi walizotoa kwa raia kwa kasi jinsi walivyopitisha BBI, kaunti hiyo ingekuwa imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo.

Suala lingine ambalo wafuasi wa Bw Odinga wanafaa kujiuliza wanapopitisha mswada huo upesi, ni kwa nini kaunti ya Kiambu au zile za Mlima Kenya bado zinachukua muda kabla ya kujadili, kupokea maoni ya umma na kupitisha mswada huo?

Je, BBI itawanufaisha wakazi wa Nyanza kuliko maeneo mengine ndiposa waikumbatie kwa kasi ya kutiliwa shaka hivyo?

Ukweli ni kwamba kaunti zitakazopitisha au kuangusha mswada huo, zitafanya hivyo si kwa sababu ripoti hiyo ni nzuri kwao au itawaletea manufaa tele, bali kwa sababu inaungwa mkono na Bw Odinga au Rais Kenyatta na kwa upande mwingine inapingwa na Naibu Rais.

BBI si suluhu kwa kila jambo nchini na haitashangaza iwapo wanasiasa wenyewe watarejea kwa raia miaka inayokuja wakitaka katiba ibadilishwe tena kukidhi tamaa zao.

Hata kama ni kuonyesha utiifu kwa vigogo wa kisiasa, ni vyema kwa kaunti kushirikisha wananchi kuhusu kufahamu mengi yaliyomo ndani ya BBI kisha mswada wake upitishwe au uangushwe kulingana na hoja zilizopo.

Habari zinazohusiana na hii