Korti yapiga Reggae ‘pause’

Na WAANDISHI WETU

MCHAKATO wa kufanikisha marekebisho ya katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) Jumatatu ulipata pigo kubwa baada ya mahakama kuagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusitisha mipango yoyote ya kufaulisha harakati hiyo hadi kesi zilizowasilishwa kortini kuihusu zisikilizwe na kuamuliwa.

Mahakama Kuu iliagiza IEBC isiendeleze shughuli zozote za kuandaa kura ya maamuzi hadi wakati kesi saba za kupinga kura hiyo zitakapoamuliwa.

Majaji watano George Odunga, Profesa Joel Ngugi, Jairus Ngaah, Enock Chacha Mwita na Janet Mulwa walisema agizo lao halijaelekezwa kwa mabunge.

Wakili Paul Mwangi alisema agizo hilo halitaathiri shughuli za kuhamasisha umma na vile vile, mjadala wa mswada huo katika mabunge ya kaunti.

Hii ina maana kuwa iwapo shughuli ya mabunge -ya kaunti na kitaifa- yatakamilisha kuidhinisha mswada huo kabla ya kesi hizo saba kukamilika, basi harakati ya kuandaa kura ya maamuzi itachelewa.

Kura ya maamuzi imeratibiwa kufanyika hapo Juni 2021.

Hayo yanajiri huku viongozi mbalimbali wanaounga mkono marekebisho ya katiba, wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga, wakiendelea kuvumisha marekebisho ya katiba.

Baada ya kukamilisha kampeni zake katika eneo la Turkana hapo wikendi, Bw Raila jana Jumatatu alikuwa Kisumu kwa dhamira ya kuwahimiza viongozi wa ukanda wa Luo Nyanza kuipigia BBI debe mashinani.

William Ruto

Kwingineko, hatua ya Naibu Rais, Dkt William Ruto kutotangaza wazi msimamo wake kuhusu ripoti ya BBI imeyaacha mabunge katika kaunti zinazomuunga mkono kwenye njiapanda kuhusu mchakato huo.

Hapo Jumatatu, Dkt Ruto alikutana na zaidi ya wabunge 130 wanaomuunga mkono kwenye makazi yake ya Karen, Nairobi, ambapo licha ya kuwahutubia wanahabari, hawakueleza msimamo wao rasmi kuihusu ripoti hiyo.

Badala yake, walishinikiza uwepo wa majadiliano kuhusu vipengele tata ili kuwaepushia Wakenya ‘mzigo’ wa kushiriki kwenye kura ya maamuzi yenye mirengo ya ‘La’ na ‘Ndiyo’.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Kitaifa, Bw Aden Duale, alisema huo ndio wanaamini kuwa mwelekeo bora utakaomfaa kila mmoja.

“Bado tunaamini kuna nafasi ya wadau wote kubuni mwafaka kuhusu mapendekezo tata kwenye ripoti,” akasema Bw Duale, ambaye pia ndiye mbunge wa Garissa Mjini.

Katika ngome yake eneo la Rift Valley, madiwani wengi wanangoja mwelekeo atakaotoa, ikiwa hakutakuwepo na muafaka rasmi kuihusu ripoti hiyo.

Mabunge ya kaunti kote nchini yanatarajiwa kuanza kuujadili mswada unaohusu ripoti hiyo wiki hii.

Duru zilisema kuwa kimya cha Dkt Ruto kimewakanganya madiwani wengi katika ngome zake, ambapo ingawa wanapanga kuwaita wananchi kuwasilisha maoni yao, wengi hawajui mwelekeo watakaochukua.

“Unajua Dkt Ruto hajajitokeza wazi kuihusu ripoti hii. Hivyo, madiwani wengi hawafahamu msimamo watakaochukua kwani hawataki kuhitilafiana naye,” zikaeleza duru katika Bunge la Kaunti ya Nandi.

“Msimamo wetu utalingana na mwelekeo utakaotolewa na Dkt Ruto,” akasema Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin-Gishu, David Kiplagat.

Madiwani watatekeleza jukumu muhimu kwenye mchakato huo, kwani lazima wajadili na kupitisha mapendekezo hayo kabla ya refarenda kufanyika.

Madiwani wengi katika eneo hilo walisema watafuata matakwa ya wananchi, wala hawatashawishiwa na misimamo au kauli za wanasiasa.

Wanataka ripoti hiyo itenganishwe na siasa za urithi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, na badala yake kuangaliwa kwa msingi wa jinsi Wakenya watakavyofaidika itakapopitishwa.

Kiongozi wa Wengi katika Kaunti ya Uasin Gishu, Josphat Lowoi, alisema baada ya kuupokea mswada huo, watawashirikisha wananchi ili kutoa maoni yao.

“Kwa sasa, tunashauriana ili kufanya maamuzi yetu bila vishawishi au shinikizo za aina yoyote ile,” akasema.

Ripoti ya Onyango K’Onyango, Wanderi Kamau na Richard Munguti

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?