• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Jinsi miiba ya ‘Mathenge’ inavyoangamiza korongo ziwani Bogoria

Jinsi miiba ya ‘Mathenge’ inavyoangamiza korongo ziwani Bogoria

Na RICHARD MAOSI

KWA muda sasa miti aina ya Mathenge inayostawi kando ya Ziwa Bogoria, Kaunti ya Baringo imekuwa kero ikizingatiwa kwamba miiba yake inaangamiza maelfu ya korongo.

Katika mazungumzo ya awali na Serman Kioko anayefanya kazi katika mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru, aliambia Taifa Leo kuwa mbali na kuwa kivutio kikubwa cha utalii katika Bonde la Ufa, safari za korongo katika maziwa ya Nakuru, Baringo na Bogoria zina mchango mkubwa katika sekta ya utalii.

Lakini utashangaa hii leo ukizuru Ziwa Bogoria ambapo utakuta idadi kubwa ya korongo walionaswa wakiwa wamekufa baina ya mashina ya miti ya ‘Mathenge’.

Kwa kawaida ndege hawa huwa wametamalaki sehemu kubwa ya ziwa, na wakati mwingine kufikia makazi ya watu, hili linajiri tangu kiwango cha maji kupanda katika Ziwa Bogoria na kuwasukuma korongo vijijini ambapo wanaishi na watu.

Baadhi ya korongo wameelea juu ya maji na wengine baina ya mashina ya ‘Mathenge’ wasiweze kujiokoa.

Baadhi ya korongo wamekuwa wakinaswa baina ya miiba ya miti aina ya ‘Mathenge’. Picha/ Richard Maosi

Ingawa wakazi wanasema mara nyingi korongo wamekuwa wakisombwa na mawimbi ya maji au kuanguka juu ya miti wanapojaribu kupaa.

Alex Kiprono ambaye ni mfugaji wa ng’ombe anasema mimea ya ‘Mathenge’ ina miiba yenye sumu hatari kwa mifugo na binadamu.

Amekuwa akizuru fuo za Ziwa Bogoria kutafutia mifugo wake nyasi, akidai kuwa sehemu hii ina chemichemi na vyanzo vya maji vyenye lishe ya kutosha ya nyasi.

Baadhi ya korongo wamekuwa wakinaswa baina ya miiba ya miti aina ya ‘Mathenge’. Picha/ Richard Maosi

Anasema kuwa siku moja aliwahi kukanyaga mwiba wa mathenge bila kujua yapata miaka miwili iliyopita, na alifikiria angepata nafuu haraka, lakini mpaka sasa bado anauguza kidonda.

Alieleza kuwa sio yeye tu, kwani baadhi ya wakazi hapa walikuwa wamekatwa miguu majeraha kutokana na miiba ya mathenge yalipokataa kupona na kusababisha vidonda.

“Inasikitisha kuona idadi kubwa ya korongo wakiangamia kila siku, wanapojaribu kutua au kupaa katika ufuo wa ziwa Bogoria,”akasema.

Kiprono anasema jeraha linalosababishwa na mti wa mathenge aghalabu huchukua muda mrefu kutibika, ikizingatiwa kuwa wakazi wengi hapa hutumia miti ya kiasili kujitibu.

Hata hivyo anaomba Wizara ya Utalii kung’oa miti hii ufuoni mwa Ziwa Bogoria ili korongo wapate fursa nzuri ya kupaa na kutafuta lishe bila vizingiti.

Idadi ya Mathenge inazidi kukaribia ziwa Bogoria, kutokana na kiwango cha maji kupanda sio tu katika ziwa Bogoria , bali pia katika ziwa Nakuru na Baringo.

Mmea huu ambao ulipandwa katika eneo la Bogoria miaka ya themanini ililenga kukabiliana na jangwa la Baringo, vilevile kuwasaidia wakazi kupata kuni na makaa.

Ni mmea ambao unaweza kufanya vyema katika maeneo kame, ila madhara yake yalianza kuonekana 1997 kutokana na mvua ya El-nino.

You can share this post!

KWA KIFUPI: Chanjo ya kukabiliana na aina mpya ya corona...

Korti yapiga Reggae ‘pause’