• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Atletico Madrid wakabwa koo na Celta Vigo huku Luis Suarez akiongoza orodha ya wafungaji bora La Liga

Atletico Madrid wakabwa koo na Celta Vigo huku Luis Suarez akiongoza orodha ya wafungaji bora La Liga

Na MASHIRIKA

LUIS Suarez alifunga mabao mawili japo hayakusaidia Atletico Madrid kusajili ushindi dhidi ya Celta Vigo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyowakutanisha uwanjani Wanda Metropolitano mnamo Februari 8, 2021.

Santi Mina aliwaweka Celta Vigo uongozini katika dakika ya 13 kabla ya Suarez kusawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Suarez ambaye ni raia wa Uruguay aliwarejesha waajiri wake Atletico uongozini katika dakika ya 50 baada ya kukamilisha krosi ya kiungo Renan Lodi.

Goli hilo la Suarez lilitazamiwa kuwapa Atletico ushindi wao wa 17 ligini ila Facundo Ferreyra akasawazishia Celta Vigo katika dakika ya 89.

Sare hiyo ina maana kwamba Atletico ambao wamepoteza mchuano mmoja pekee wa La Liga kufikia sasa msimu huu, wanajivunia alama 51 kileleni mwa jedwali huku pengo la pointi nane likitamalaki kati yao na Barcelona ambao wamejizolea idadi sawa ya alama na mabingwa watetezi, Real Madrid.

Hata hivyo, nafuu zaidi kwa Atletico wanaonolewa na kocha Diego Simeone ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimetandazwa na washindani wao wakuu wakiwemo Barcelona, Real na Sevilla wanaofunga mduara wa nne-bora kwa pointi 42.

Suarez aliyebanduka Barcelona na kutua Atletico mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20, sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa La Liga kwa mabao 16 kutokana na mechi 20 kufikia sasa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ingwe yapata mpinzani mpya Betway Cup timu ya Taita Taveta...

Ghost afurahishwa na vijana wake wa Harambee Stars mazoezini