• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Sonko apelekwa kortini kwa ambulensi

Sonko apelekwa kortini kwa ambulensi

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko amefikishwa katika mahakama ya Kiambu kwa ambulensi kutoka hospitali alimolazwa Jumatatu baada ya kuugua akiwa rumande.

Polisi walifika katika hospitali hiyo na kumuondoa kumpeleka kortini wakisema hali yake haikuwa mbaya sana. Mawakili wake walisema kwamba ambulensi hiyo ilikuwa na daktari na vifaa vya kumhudumia mwanasiasa huyo hali yake ya afya ikidorora.

Haikubainika iwapo madaktari walimruhusu kuondoka hospitalini lakini duru zilisema hawakutaka polisi kuzua kizaazaa walipofika kumchukua Sonko.

Sonko alilazwa baada ya kulalamikia maumivu ya tumbo akiwa rumande katika kituo cha polisi cha Gigiri.

Ilisemekana kuwa alikuwa na shinikizo la damu pia.

Mwanasiasa huyo alitarajiwa kortini Jumanne mawakili wake walipotangaza kwamba alikuwa amelazwa hospitali.

Polisi walipopata habari hizo walienda kumchukua na kumpeleka kortini mwendo wa saa tano na dakika 15 mchana.

Awali Jumanne wakili wake John Khaminwa alikuwa amesema kwamba wangejaribu kufikisha Sonko kortini alivyoagizwa.

Kutoka mahakama ya Kiambu anakokabiliwa na kesi ya kushambulia na wizi wa mabavu, Sonko anatarajiwa katika Mahakama ya Kahawa anakokabiliwa na madai ya kuhusika na ugaidi.

Maafisa wa upelelezi wa uhalifu wanasema kwamba wana habari Sonko alikuwa akihusika na vitendo vya kigaidi. Wanaomba mahakama iwaruhusu wamzuilie kwa siku 30 ili wakamilishe uchunguzi.

Wasaidizi tisa wa Bw Sonko pia wamekamatwa kuhusiana na madai hayo.

Sonko amekuwa akilalamika kuwa maisha yake yamo hatarini akidai maafisa wa polisi walijaribu kumdunga sumu akiwa seli.

Upande wa mashtaka umeomba asiachiliwe kwa dhamana ukidai anaweza kutoroka alivyofanya 2001 katika kesi iliyomkabili Mombasa.

Bw Sonko amekanusha madai hayo.

You can share this post!

Ghost afurahishwa na vijana wake wa Harambee Stars mazoezini

Bayern Munich yadengua Al Ahly na kufuzu kwa fainali ya...