• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:11 PM
TAHARIRI: Elimu: Mtaala mpya wahitaji ushirikiano

TAHARIRI: Elimu: Mtaala mpya wahitaji ushirikiano

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI ya jopokazi lililoshughulikia mageuzi katika mtaala wa elimu iliyokabidhiwa Rais Uhuru Kenyatta jana inatoa mapendekezo muhimu yanayohitaji ushirikiano wa wadau wote katika sekta hiyo.

Ushirikiano huu hautaweza kuepukwa iwapo mtaala huo utatimiza malengo yake ya kufanya wanafunzi kuwa raia wema, wanaojiamini na kujitambua huku wakijijenga kimaisha na kustawisha nchi yao.

Tofauti na mfumo unaotumika kwa sasa wa 8-4-4, mtaala huo unazingatia uwezo wa mwanafunzi katika taaluma na nyanja tofauti. Uwezo huo hautatathminiwa kupitia mitihani ya kitaifa inavyofanyika kwa wakati huu ni kupitia ukuzaji wa talanta na ubunifu.

Hii itafanya mwalimu kuwa mwelekezi na mshauri mkuu katika utekelezaji wa mtaala huo akisaidiana na wazazi na jamii kwa jumla.

Ikiwa kila mmoja atashiriki kuufanikisha bila shaka utakapotekelezwa kikamilifu utachangia kufanya Kenya kuwa nchi bora yenye wataalamu na watafiti wa hali ya juu.

Jamii itahitaji kutambua kwamba elimu sio inayotolewa darasani pekee, wanafunzi watakuwa na maadili mema kwa kutambua majukumu yao kama raia.

Inatia moyo kuona Rais Kenyatta amebuni idara ya kufuatilia utekelezaji wa mabadiliko katika sekta ya elimu kwa lengo ya kuhakikisha changamoto zitakazoibuka zitashughulikiwa kikamilifu.

Wazazi wanafaa kuunga mtaala huu kwa kuwa utahakikisha hakuna mwanafunzi atakosa kuendelea na masomo, nao wanafunzi watakuwa na hakika kwamba hawatakatiza masomo kwa kufeli mitihani ya kitaifa inayowafanya kukosa imani katika maisha.

Manufaa ya mtaala huu ni kuwa kila mwanafunzi atakuwa mshindi kivyake. Kwa kuwa ni mtaala mpya basi, serikali haina budi kuhakikisha walimu wamepata mafunzo kuuhusu.

Wengi wa walimu wanaofunza katika shule kwa wakati huu wamefunzwa kuhusu mfumo wa 8-4-4 waliousoma kuanzia chekechea na kuna haja ya kuhamasishwa kuhusu mtaala huu mpya ambao kwa sasa utekelezaji wake umefikia Gredi ya Nne.

Kwa kuwa unalenga kuhakikisha kuna usawa katika upatikanaji wa elimu, serikali inafaa kuhakikisha mapendekezo yote ya jopokazi yanatekelezwa kikamilifu katika maeneo yote nchini.

Elimu ndiyo nguzo ya uchumi wa nchi na sekta hiyo ikinawiri, nchi nzina itapata maendeleo. Ripoti hiyo imesisitiza walimu, wazazi na jamii kwa jumla ni nguzo kuu katika ufanikishaji mtaala huu hivyo basi hawana budi kuwajibika na kushirikiana kufikia ndoto hii.

You can share this post!

Urithi wa Mvurya waibua joto zaidi

COVID-19: Mechi za Europa League kati ya Real Sociedad na...