• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Juventus yadengua Inter Milan na kuingia fainali ya Coppa Italia kwa msimu wa pili mfululizo

Juventus yadengua Inter Milan na kuingia fainali ya Coppa Italia kwa msimu wa pili mfululizo

Na MASHIRIKA

JUVENTUS walifuzu kwa fainali ya Coppa Italia msimu huu kwa jumla ya mabao 2-1 kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza baada ya kuambulia sare tasa kwenye marudiano ya nusu-fainali mnamo Jumanne usiku.

Juventus wa kocha Andrea Pirlo walishuka dimbani katika uwanja wao wa nyumbani wakijivunia ushindi wa mabao mawili ya ugenini kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza jijini Milan wiki moja iliyopita.

Kwa kuwadengua Inter ya kocha Antonio Conte, Juventus kwa sasa wamefuzu kwa fainali ya Coppa Italia kwa msimu wa pili mfululizo.

Fowadi wa zamani wa Everton na Manchester United, Romelu Lukaku pamoja na Achraf Hakimi walipoteza nafasi mbili za wazi ambazo vinginevyo, zingewapa Inter ushindi wa mabao mawili kwenye mchuano huo wa mkondo wa pili.

Cristiano Ronaldo naye alishuhudia makombora yake mawili yakipanguliwa na kipa Samir Handanovic wa Inter.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza, Inter walitangulia kuona lango la Juventus kupitia bao la fowadi raia wa Argentina, Lautaro Martinez kabla ya Ronaldo kupachika wavuni mabao mawili chini ya dakika tisa za mwisho wa kipindi cha pili.

Juventus kwa sasa watakutana na mshindi wa nusu-fainali ya pili itakayowakutanisha leo Atalanta na Napoli walioambulia sare tasa kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wiki iliyopita jijini Naples. Fainali ya Coppa Italia msimu huu imeratibiwa kufanyika Mei 19, 2021.

Napoli waliwachabanga Juventus 4-2 kupitia penalti kwenye fainali ya Coppa Italia mnamo 2019-20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid wapiga Getafe na kukaribia Atletico kileleni...

Nikosoe nikung’ate