NGILA: Ndoto ya Afrika yafa kwa kuzimiwa intaneti

Na FAUSTINE NGILA

AFRIKA kuna taabu. Kuna uozo wa fikra hasa katika mpango mzima wa kuunganisha mataifa yote 54 kuwa soko la pamoja la kidijitali.

Nimepitia ripoti ya kampuni ya utafiti wa intaneti ya Comparitech, na ninachosoma kinaanika ukosefu wa uelewa wa mustakabali wa uchumi wa bara hili.

Je, wajua kwamba kwa siku tano ambazo taifa la Uganda lilizimia raia wake intaneti eti kwa kuwa Rais Museveni alinuia kushinda urais, lilipoteza Sh1 bilioni?

Kulingana na utafiti huo, ninapata kuwa hizo ni hela kidogo ikilinganishwa na Tanzania ambayo ilizima intaneti kwa saa 1584 mwaka uliopita. Matokeo? Taifa la John Magufuli lilipoteza Sh63 bilioni katika kipindi cha uchaguzi.

Nchini Chad, Sh2.6 bilioni ziliyeyuka kwa kutoa mawimbi ya intaneti kwa saa 3900 kuanzia Julai hadi mwishoni mwa mwaka.

Ethiopia nayo, kutokana na mapigano eneo la Tigray, ilizima intaneti kwa zaidi ya saa 3,600 na kupoteza Sh11 bilioni.

Inashangaza kuwa duniani kote, Afrika ndiyo inasalia gizani kwa kipindi kirefu zaidi mitandaoni, licha ya juhudi za mataifa yaliyoendelea kujaribu kueneza intaneti mashinani mwa bara hili.

Marais sasa wanatumia intaneti kama silaha wakati wa uchaguzi au machafuko, wanaonekana kuwa mbioni kukatiza uhuru wa wananchi kutuma na kupokea taarifa kuhusu taifa lao mitandaoni, hali ambayo inaua demokrasia.

Wasichojua ni kwamba kwa kufanya hivi, wanafukuza wawekezaji wengi mno wanaotegmea intaneti kufanya biashara, huku pia wakiwavunja moyo wale ambao wana mipango ya kuwekeza katika bara hili.

Uchumi wa sasa unaendeshwa kwa intaneti, na inashangaza Afrika inarudi katika zama za kale ambapo viwanda vilitegemea mvuke au upepo.

Hata wakati wa mashindano ya kisiasa katika uchaguzi, tunafaa kujifunza kutokana na Amerika ambayo licha ya juhudi za Donald Trump kujaribu kusalia mamlakani, asasi kuu hazingeruhusu intaneti kufungwa maanake uchumi wake wote unategemea mitandao.

Afrika inafaa kung’amua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, na kitendo cha kuwanyima wananchi na wafanyabiashara intaneti ni pigo kuu wakati huu ambapo Umoja wa Afrika unajaribu kuunda soko la pamoja mitandaoni ili kuwa na usemi katika uchumi wa dijitali duniani.

Utawezaje kununua bidhaa mitandaoni nchini Uganda, Tanzania, Ethiopia au Chad wakati mataifa hayo yameamuru intaneti izimwe? Ukinyimwa intaneti ni sawa na kunyimwa Oksijeni ya kupumua, ni sawa na kuuawa.

Kila kitu sasa kinategemea intaneti, iwe ni elimu, kilimo, uchukuzi, mawasiliano au afya, hasa katika kipindi hiki ambapo janga la corona limetufunza kutumia teknolojia kupambana na changamoto mbalimbali.

Na iwapo nia ni kuwatia adabu wapinzani wa uchaguzi mkuu, basi demokrasia barani Afrika itasalia ndoto kwa miaka mingi ijayo. Utafika wakati ambapo wananchi watajua jinsi ya kutumia intaneti ya siri na kinachofichwa kwenye giza la intaneti kiwekwe wazi.

Lazima mzaha huu ukome. Afrika itajificha chini ya kauli ya ‘kulinda usalama wa kitaifa’ lakini ukweli ni kuwa inasambaratisha uchumi wake wa kidijitali ambao tayari unapata dhoruba kali kutoka mabara yaliyoendelea. Inshangaza badala ya kuongeza mgao wake katika uchumi wa mitandaoni, Afrika inapunguza.

Habari zinazohusiana na hii