WASONGA: Viongozi wajadili masuala yanayoathiri raia moja kwa moja

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE, maseneta na madiwani, kama wawakilishi wa umma, hutekeleza wajibu mkubwa zaidi katika nchi zinazokumbatia demokrasia-wakilishi kama Kenya.

Kando na kutunga sheria na kufuatilia utendakazi wa serikali, wao huwasilisha matakwa ya raia kwa asasi za uongozi.

Hii ndio maana wawakilishi hawa wanaporejelea vikao vya kawaida wiki hii baada ya likizo ndefu ya miezi miwili, wananchi wanatumai kuwa watatumia fursa hiyo kujadili masuala yanayowaathiri moja kwa moja, nyakati hizi ngumu.

Kwanza, ni matumaini yangu kwamba viongozi hawa watashughulikia kwa kina changamoto zinazoathiri sekta ya afya wakati huu ambapo wengi wa wahudumu wa afya wamegoma wakilalamikia mahitaji mbalimbali wakati huu wa janga la corona.

Wasitumie kumbi za mabunge yao kama majukwaa ya kuchapa siasa za kura ya maamuzi kuhusu mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano BBI na siasa za urithi wa kiti ya urais.

Wananchi ambao ndio wanaowategemea wawapigie kura mwaka ujao, wamekuwa wakiteseka kwa kukosa matibabu katika hospitali za umma.

Katika bunge la kitaifa, wabunge watambue kuwa huu ni wakati muhimu zaidi kwa kuzamia shughuli ya utayarishaji bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2021/2022 na mijadala kuhusu miswada ya ugavi wa mapato kwa serikali za kaunti.

Wazingatie kuwa watakuwa wakitekeleza kibarua hicho muhimu wakati ambapo uchumi wa Kenya unakabiliwa na changamoto nyingi zilizosababishwa na janga la Covid-19. Kwa hivyo, wanapaswa kuwa makini zaidi wanapogawa fedha kwa sekta mbalimbali za kiuchumi.

Kupitia Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega, ni muhimu ikiwa wabunge watatenga fedha nyingi katika sekta za kuinua uchumi.

Sekta kama kilimo, utalii, elimu na usalama zinahitaji kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya kitaifa. Hii ni kwa sababu sekta hizi ni miongoni mwa zile ambazo ziliathirika zaidi na janga la corona tangu Machi 2020.

Vile vile, wabunge na maseneta wakomeshe huu mtindo wa wao kuvutana kuhusu Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Serikali Kuu na zile za Kaunti. Katika miaka miwili ya kifedha iliyopita, vuta nikuvute kati ya wabunge na maseneta imetumbukiza kaunti katika shida za kifedha baada ya Hazina ya Kitaifa kuchelewa kusambaza fedha kwa serikali hizo.

Kimsingi, wabunge, maseneta na madiwani wana wajibu mkubwa kwa umma wakati huu wanaporejelea vikao na hivyo wanapaswa kuweka masilahi ya umma mbele wala sio matakwa yao finyu.

Habari zinazohusiana na hii